Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imesema inaendelea kufanya marekebisho ya kisheria yaliyotengwa kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto huku ikiweka wazi kuwachukulia hatua wale wote watakao telekeza familia hata kama ni watumishi wa umma.
Hayo yameelezwa leo Mei 8,2025 Jijini Dodoma na Waziri wa maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum,Dk.Dorothy Gwajima wakati akitoa tamko kuhusu siku ya familia kimataifa huku akiwataka wazazi kutenga muda na kuwa na utamaduni wa kuzungumza na watoto wao.
“Tunashuhudia baadhi ya familia zinaendeleza mifarakano na migogoro ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika malezi, makuzi na ustawi wa watoto katika familia.”amesema Dkt.Gwajima
Dkt.Gwajima amesema kuwa moja ya vichocheo vya migogoro katika familia ni kukosekana kwa upendo, ustahimilivu na kutokuwa na hofu ya Mungu miongoni mwa wenza na wanafamilia.
“Mifumo kandamizi inayoendelea katika baadhi ya jamii inayochochewa na mila na desturi zenye madhara za baadhi ya makabila hapa nchini imeendeleza ukatili wa kijinsia kati ya wenza au wanandoa jambo ambalo lina athari kubwa katika malezi na ustawi wa watoto, familia na jamii kwa ujumla.”amesema Dkt.Gwajima
Aidha amesema kuwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wengi wamekimbia familia zao kutokana na migogoro ya wenza au wanandoa.
Sambamba na hayo ameeleza kuwa kumekuwa na ugumu kwa wanandoa au wenza kukubali kujadili na hatimaye kumaliza tofauti zao. Hali hii imesababisha ndoa na mahusiano mengi kuvunjika. Mara zote waathirika wakubwa wamekuwa ni watoto.
“Kwa sasa tunashuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili miongoni mwa watoto na kujiingiza katika vitendo visivyo na tija kwa familia, jamii na taifa; mathalani; matumizi ya dawa za kulevya na kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo vimesababisha ongezeko la maambukizi ya VVU kwa kundi la watoto na vijana balehe.”amesema
Amesema kuwa Serikali imeendeleza jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja kuwaomba viongozi wa dini kuimarisha mafundisho kwa wanandoa kabla na baada ya kuingia kwenye taasisi hiyo muhimu ili kunusuru mifarakano inayopelekea ongezeko la ndoa kuvunjika.
“Wizara yake kwa kushirikiana na viongozi wa dini, imeandaa vitabu vya malezi ya watoto kwa muktadha wa dini ya kikristo na kiislam vinavyojulikana kwa jina la wazazi wangu kesho yangu ili kuwaelimisha waumini wa dini hizo namna ya kulea watoto wakiwa na hofu ya Mungu.”amesema.
Hata hivyo,Dk.Gwajima amebainisha kuwa katika kukabiliana na makosa ya ukeketaji atakayebainiwa atatozwa faini ya Shilingi milion 2 au kifungo kisichopungua miaka mitano au miaka 15.
No comments:
Post a Comment