ULEGA AAGIZA UCHUNGUZI WATENDAJI BRT4 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

ULEGA AAGIZA UCHUNGUZI WATENDAJI BRT4


Na Mwandishi Wetu


WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kupelekewa taarifa kamili za wasimamizi na mshauri elekezi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne baada ya kushuhudia uzembe unaosababisha usumbufu zaidi barabarani kinyume na malengo ya mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo unaotoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mwenge hadi Tegeta, sambamba na sehemu ya kutoka Mwenge hadi Ubungo, Ulega alieleza kushangazwa na jinsi wasimamizi na mshauri elekezi wa mradi huo wanavyoonekana kufumbia macho uzembe huo.

Mojawapo ya maeneo ambayo yalimkera waziri huyo ilikuwa ni katika eneo la Palm Beach, Upanga ambako alikuta shimo kubwa limechimbwa na mkandarasi, pasipo kukamilisha kwanza kazi ya muhimu zaidi katika maeneo ya awali kutoka Morocco hadi Mwenge hadi Kaunda.

“Mimi nimepita kukagua. Kazi ambazo nimeaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni za barabara na madaraja. Rais hapendi na hafurahishwi na msongamano mkubwa hapa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Hisia hizo hajawahi kuzificha,” alisema Waziri Ulega.

Ameongeza kuwa alipohoji sababu ya kuchimba eneo jipya kabla ya kukamilisha maeneo ya awali, alielezwa kuwa ni mkandarasi huyo huyo ambaye bado hajamaliza kazi sehemu ya mwanzo.

“Nini kimemfanya awe na haraka ya kuja kutifua huku wakati kule hajakamilisha? Hii ndiyo hoja yangu na ugomvi wangu hapa,” alisema.

Waziri Ulega amesema amebaini tatizo kubwa liko kwa upande wa wasimamizi wa mradi pamoja na Mshauri elekezi. 

“Hii ni barabara ya umma, si mali ya mkandarasi. Mkandarasi hawezi kuvamia na kuchimba kiholela. Hapa shida si mkandarasi peke yake, ni wasimamizi na mshauri elekezi,” alisema kwa msisitizo.

Kutokana na alichokishuhudia, Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kumletea taarifa kamili za wasimamizi wote pamoja na Mshauri Elekezi kwa ajili ya uchunguzi, akisema aina ya uzembe alioushuhudia inaonyesha kuna jambo lingine la ziada limejificha na si uzembe wa kawaida.

“Haiwezekani ikawa tu ni uzembe wa kawaida, inaweza kuwa kuna jambo linafichwa,” aliongeza.
Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, alisema kama waziri ana mamlaka ya kumnyang’anya mkandarasi baadhi ya maeneo kama ataonekana kushindwa kwenda na kasi ya serikali na hatasita kuyatumia pale itakabobidi.

“Yawezekana wale wanaotakiwa kunishauri kwa uaminifu, wamehamia upande wa mkandarasi. Kazi yao ni kunisaidia, si kuficha uzembe,” alieleza.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi Rajabu Iddi amewaomba radhi wananchi kwa usumbufu wanaoupata, akisema wanaendelea kusimamia mradi huo kwa juhudi kubwa kuhakikisha unakamilika kwa wakati. 

Mhandisi Rajab ameeleza kuwa wanaweka mikakati ya kupunguza usumbufu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na matangazo na njia mbadala.

Mradi wa BRT Awamu ya Nne sehemu ya kwanza una jumla ya vituo 18 vya mwendokasi, na unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam pindi utakapo kamilika.

No comments:

Post a Comment