
Na Anangisye Mwateba, Dodoma
Jumla ya wananchi 1,640 kutoka vijiji vya Engikaret na Kiserian, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, wamepatiwa elimu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum Mhe. Zaytun Seif Swai ambaye amehoji mkakati wa Serikali katika kukabiliana na tembo waliovamia Kata ya Engikaret ili kulinda usalama wa wananchi.
Mhe. Kitandula akijibu swali hilo, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti changamoto hiyo, ikiwemo kufanya doria za mwitikio wa haraka na kwamba tangu Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya doria 34 za kudhibiti matukio ya wanyamapori wakali zimefanyika Kata ya Engikaret.
Aidha, ameongeza kuwa mwaka 2021 Serikali ilijenga kituo maalum cha askari katika Wilaya ya Longido kwa lengo la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, hasa tembo. Kituo hicho kina jumla ya askari 18, wakiwemo wahifadhi 8 na askari wa wanyamapori wa vijiji (VGS) 10.
Kwa mujibu wa Mhe. Kitandula, kituo hicho pia kimewezeshwa kwa vitendea kazi vikiwemo gari moja na pikipiki nne, vinavyotumika kuimarisha ulinzi na kudhibiti matukio ya wanyamapori wakali katika vijiji vya Engikaret na Kiserian, Kata ya Engikaret.

No comments:
Post a Comment