
Mbunge wa viti maalum Mhe. Ester Amos Bulaya amemtaja Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na Naibu Waziri Kundo Mathew kama Viongozi wenye unyenyenyekevu wa pekee, wenye kufikika na wenye kuzingatia maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Wabunge na wadau mbalimbali wa sekta ya maji nchini.
Akichangia Mjadala wa hotuba ya Wizara ya maji kwa mwaka 2025/26, Bulaya amempongeza pia Mkurugenzi wa Idara ya Maji Wilayani Bunda Mkoani Mara na Timu nzima ya Wizara ya Maji, akisema wamefanikiwa pakubwa kutekeleza miradi ya maji na kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Katika maelezo yake. Bulaya kadhalika ameitaka Wizara hiyo kusimamia kikamilifu ulipwaji wa madeni ya zaidi ya Bilioni 61 zinazodaiwa kwa Taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Jeshi la Magereza, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi na Wizara mbalimbali ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza miradi ya maji nchini.
"Sekta ya maji ni muhimu, maji ni hitaji la msingi, miradi inawezaje kukamilika kama fedha haitoki?miradi ya maji inawezaje kukamilika kama taasisi za serikali zinakaa na Bilioni 61? Hivi hela hizi zingetoka watu wangu wa Nyamatoke wangepata maji,watu wangu wa Misisi wangepata maji, watu wangu wa Chenguge wangepata maji" Amesema Mhe. Bulaya.
Mheshimiwa Bulaya pia amewataka wabunge na Wizara ya Maji kushinikiza kulipwa fedha za mfuko wa maji kutoka kwa Wizara ya Maji, akieleza kuwa ni matarajio yake kwamba Bajeti zinapopitishwa Bungeni ni kazi ya Wizara ya fedha kutoa fedha haraka ili kwenda kuhudumia wananchi wenye changamoto za upatikanaji wa maji.


No comments:
Post a Comment