
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), amewasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambapo Wizara hiyo imeomba jumla ya Shilingi 76,057,153,000.00 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Katika hotuba yake, Mhe. Gwajima amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 49,115,697,000.00 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ikiwa ni pamoja na Shilingi 22,646,148,000.00 kwa mishahara ya watumishi na Shilingi 26,469,549,000.00 kwa matumizi mengineyo.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri amesema Wizara inakadiria kutumia Shilingi 26,941,456,000.00, ambapo Shilingi 15,415,404,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 11,526,052,000.00 ni fedha kutoka kwa wahisani wa maendeleo.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara inatarajia kukusanya maduhuli ya Shilingi 7,040,129,000.00 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vilivyoainishwa.
Mhe. Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa bajeti hiyo inalenga kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha usawa wa kijinsia, kulinda haki za wanawake na watoto, pamoja na kuendeleza makundi maalum ili kufikia maendeleo jumuishi kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
No comments:
Post a Comment