
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, Juni 28, 2025, amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Asia Abdallah amesema kuwa uamuzi wake umetokana na dhamira ya dhati ya kuwaletea wanawake wa Mkoa wa Dodoma maendeleo endelevu. Amewataka wanawake kuchukua nafasi zao ipasavyo katika uongozi wa nchi, akisisitiza kuwa muda umefika kwa wanawake kuwa mstari wa mbele katika uongozi na ustawi wa jamii.
Kauli mbiu yake katika kinyang’anyiro hicho ni:
“Tumaini Jipya la Wanawake Mkoa wa Dodoma,”
ikiwa ni wito wa matumaini mapya, usawa wa kijinsia, na ustawi wa wanawake katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Asia Abdallah ni miongoni mwa viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiutendaji serikalini, akibeba uzoefu mkubwa wa uongozi pamoja na maono mapya ya kuwatumikia wananchi kwa bidii na uaminifu.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM limeanza rasmi Juni 28, 2025, na linaendelea katika mikoa yote nchini huku wagombea mbalimbali wakiendelea kujitokeza kuwasilisha nia na dhamira zao za kulitumikia Taifa kupitia chama hicho.











No comments:
Post a Comment