Katika hatua inayoonesha umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara katika maendeleo ya taifa, CFAO Mobility Tanzania imefanya makabidhiano ya awali ya malori mapya aina ya Fuso CANTER FE84 kwa Bakhresa Food Products Limited (BFPL), ikiwa ni sehemu ya mchakato wa upanuzi wa floti ya malori 100 unaolenga kuboresha usafirishaji na ufanisi wa usambazaji wa bidhaa kote nchini Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika katika kiwanda cha BFPL kilichopo Mwandege, mkoani Pwani, na kuhudhuriwa na menejimenti ya juu kutoka kampuni zote mbili, wafanyakazi, pamoja na madereva waliopata fursa ya kuendesha malori hayo kwa mara ya kwanza.
Tukio hili linadumisha uhusiano wa muda mrefu kati ya CFAO Mobility Tanzania na BFPL — ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 — na pia linaonesha faida za ushirikiano wa aina hii katika kukuza fursa za kibiashara, ajira na ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa BFPL, Salim Aziz, amesifu CFAO Mobility Tanzania kwa kuwa mshirika wa kuaminika katika kuwapatia magari imara na huduma bora baada ya mauzo.

“Tunaishukuru CFAO Mobility Tanzania kwa kuwa waaminifu na wenye kutegemewa, jambo ambalo limechangia pakubwa katika kufanikisha malengo yetu ya kiutendaji. Muhimu zaidi, malori haya mapya yataimarisha shughuli zetu za biashara na moja kwa moja yatazalisha zaidi ya ajira 200, zikiwemo nafasi kwa madereva na wasaidizi wao,” alisema.
“Hili si suala la kuongeza malori tu — ni ahadi ya kuchangia maendeleo ya taifa, ambapo kila lori linawakilisha fursa zaidi kwa watu, kuboresha maisha, na kuimarisha jamii.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Mobility Tanzania, Ali Timimi, amesifu BFPL kwa mtazamo wake wa kimaendeleo na kuwa mstari wa mbele katika kuboresha ufanisi kupitia uwekezaji wa malori mapya kabisa.
“BFPL inaonesha mfano bora wa biashara yenye uwajibikaji ndani na nje ya Tanzania. Uamuzi wao wa kuwekeza katika malori mapya kabisa unaakisi dhamira yao ya kweli ya kuwekeza katika ufanisi wa muda mrefu na uendelevu,” alisema Timimi.
“Usafirishaji wenye ufanisi ni mhimili muhimu kwa uchumi wa taifa. Biashara kama Bakhresa zinapoweka mkazo katika kuhakikisha usafirishaji wa kuaminika, manufaa yake huonekana katika mnyororo mzima wa thamani — kuanzia viwandani hadi madukani, na hatimaye kwenye kaya za Watanzania.”
Kwa kuwa kampuni hii kubwa ya uzalishaji wa chakula na vinywaji inaendelea kupanua wigo wake Afrika Mashariki, Kati na Kusini, floti hii mpya inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika kuhakikisha usambazaji wa bidhaa kwa wakati na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha kimkakati cha usafirishaji na uzalishaji wa chakula katika ukanda huu.
No comments:
Post a Comment