CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) CHASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NA KUTANGAZA FURSA ZA KIMATAIFA KWA WAHITIMU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 18, 2025

CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) CHASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NA KUTANGAZA FURSA ZA KIMATAIFA KWA WAHITIMU



Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni 2025, kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na chuo hicho katika sekta ya bahari na usafirishaji kwa njia ya maji.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho haya, DMI imeeleza jitihada mbalimbali zilizofanywa na zinazofanywa na chuo hicho katika kuhakikisha wahitimu wake wanapata ajira za ndani na kimataifa.

Akizungumzia hilo Mhadhiri Msaidizi wa DMI, Bw. Azan Azan, amebainisha kuwa chuo hicho kimeingia makubaliano na nchi tatu za Korea Kusini, Ghana na Italia kwa ajili ya kuwawezesha wahitimu wake kufanya kazi na kupata mafunzo zaidi katika sekta ya usafirishaji majini katika nchi hizo.

“Katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa wahitimu, DMI imechukua hatua ya kuingia makubaliano ya kimataifa ambayo yatafungua fursa kwa vijana wetu kupata ajira katika masoko ya kimataifa,” amesema Bw. Azan.

Aidha, ameongeza kuwa Chuo cha DMI kimeingia makubaliano na kampuni kubwa ya meli kutoka Ugiriki ya DANAOS yenye tawi lake visiwani Zanzibar hatua inayolenga kuwasaidia wahitimu kupata ajira kwa urahisi pindi wanapohitimu masomo yao, ikiwa ni sehemu ya kuchochea maendeleo kupitia uchumi wa buluu.

“DMI imejipanga kikamilifu kutoa mafunzo yanayozingatia mahitaji ya soko la ajira, pamoja na huduma za utafiti na ushauri elekezi katika taaluma za baharini na zinazohusiana kwa lengo la kuwa taasisi kinara katika sekta hii,” amefafanua.

Katika wito wake kwa Umma, Bw. Azan amewahimiza wazazi na wanafunzi kuchangamkia fursa zinazotolewa na DMI, akibainisha kuwa kozi zote zinazotolewa na chuo hicho zinahitajika sana katika soko la ajira la kitaifa na kimataifa.

Ushiriki wa DMI katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma unatoa nafasi ya kipekee kwa wananchi kufahamu kwa undani mchango wa chuo hicho katika kujenga rasilimali watu wenye ujuzi wa kitaaluma na ushindani wa kimataifa katika sekta ya bahari na uchumi wa buluu.








No comments:

Post a Comment