Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Atoa Wito wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 18, 2025

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Atoa Wito wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji


Na Angela Msimbira , IRINGA 


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Bw. Atupele Mwambene, amewataka viongozi wa elimu ngazi ya msingi na sekondari kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji ili kuboresha viwango vya ufaulu nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Tathmini ya Utekelezaji wa Shughuli za Elimu kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2025, kilichowakutanisha Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri katika viwanja vya Kichangani, mkoani Iringa, Mwambene amesisitiza umuhimu wa uongozi bora katika sekta ya elimu.

“Ni wajibu wa viongozi kusimamia kwa makini mchakato wa utoaji elimu, kuhakikisha miundombinu inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa sambamba na kuzingatia maelekezo ya mamlaka husika,” amesema.

Amehimiza pia kuimarisha ushirikiano baina ya viongozi hao na wasaidizi wao katika maeneo ya kazi, kwa kuwapatia taarifa sahihi na kuwaelekeza ipasavyo ili kwenda sambamba na falsafa ya taifa katika maendeleo ya elimu.

Aidha, amewataka viongozi hao kuendelea kutoa huduma kwa upendo na staha kwa walimu na wadau wengine wa elimu, ili kuongeza ari ya utendaji kazi.

“Walimu wanapaswa kusikilizwa, kuelekezwa na kushauriwa kulingana na changamoto walizonazo. Hii itasaidia kuongeza morali ya kazi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu,” alisisitiza Mwambene.

Kikao kazi hicho ni sehemu ya mikakati ya serikali kupitia TAMISEMI katika kuhakikisha kuwa elimu bora inapatikana kwa kila mtoto wa Kitanzania kupitia usimamizi thabiti na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa sera na mipango ya elimu nchini.

No comments:

Post a Comment