RAIS SAMIA ARIDHISHWA UJENZI WA MIUNDOMBINU JIJI LA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 14, 2025

RAIS SAMIA ARIDHISHWA UJENZI WA MIUNDOMBINU JIJI LA DODOMA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imedhamiria kuufungua Mkoa wa Dodoma kwa njia ya barabara, reli na anga ili kuufanya kuwa mji wa kisasa na kivutio cha biashara, uzalishaji na hivyo kukuza wananchi wa Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza jijini Dodoma leo Juni 14, 2025 mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma (km 112.3) na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Rais Dkt. Samia ameelezea kuridhishwa kwake na ujenzi wa miradi hiyo na kuzitaka Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi kusimamia kikamilifu miradi hiyo ili ikamilike kwa viwango vilivyosanifiwa.

“Nawapongeza Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, TANROADS, Wakandarasi na Wahandisi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo itasaidia kupunguza muda wa safari na kurahisisha usafiri na hivyo kuleta tija kwa wananchi”, ameeleza Dkt. Samia.

Dkt. Samia ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo katika kipindi cha hivi karibuni imewezesha ujenzi wa barabara ya Kabingo - Kasulu - Manyovu, Mnivata - Newala - Masasi, Namtumbo - Tunduru, Sakina - Tengeru, na barabara ya Mchepuo ya Arusha na barabara ya Tabora - Koga - Mpanda.

Aidha, Rais Dkt. Samia amemshukuru Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina kwa kuwa mbia wa kweli na mdau muhimu wa miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameeleza kuwa licha ya barabara hiyo kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji la Dodoma itaongeza fursa za kiuchumi na maendeleo kwa jamii yetu kwa kurahisissha usafiri na usafirishaji wa bidhaa pia itakuza utalii, biashara na viwanda.

Amebainisha kuwa Wizara imejipanga kukabiliana na msongamano wa magari katikati ya jiji la Dodoma kwa kuzipanua barabara ya Dodoma - Morogoro sehemu ya Chamwino- Kimbinyiko (roundabout) kuwa njia sita (km 32), barabara ya Dodoma - Iringa sehemu ya Roundabout ya Image - Nkoze kuwa njia nne (km 7.5) na barabara ya Dodoma - Arusha sehemu ya Wajenzi - Msalato kuwa njia ya nne (km 8.5).

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina ameishukuru nchi ya Tanzania kwa ukarimu wake katika kipindi cha miaka 10 alichoongoza Benki hiyo na kusisitiza kwamba katika kipindi chake zaidi ya Dola Bilioni 4.73 za kimarekani zilitolewa kuendeleza miradi ya miundombinu nchini Tanzania.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameitangaza rasmi barabara ya mzunguko wa nje wa dodoma kuanzia sasa itaitwa barabara ya Dkt. Akinwumi Adesina.




No comments:

Post a Comment