
Na WMJJWMM-Shinyanga.
Serikali inaendelea kuhakikisha Wazee wanaishi kwa usalama na kulindwa dhidi ya vitendo na aina yoyote ya ukatili kupitia afua mbalimbali ikijumlisha sera, kanuni na mikakati mbalimbali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis Juni 15, 2025 mkoani Shinyanga katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema zipo sababu tofauti za ukatili katika jamii ikiwemo mila na desturi zenye madhara, imani potofu, ramli chonganishi pamoja na baadhi ya watoto kuwatelekeza wazazi wao na kuwadhulumu mali zao.
“Ni muhimu sote tukatambua kuwa ukatili haukubaliki kwa makundi yote katika jamii zetu, hivyo ni muhimu kila mmoja wetu akawa balozi mwema, mlinzi na mtoa taarifa mara anapoona vitendo vya ukatili dhidi ya Wazee kwani taarifa zinaonesha kuwa vitendo vya ukatili dhidi yao hufanywa na ndugu pamoja na watu wa karibu wanaowaamini.” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amebainisha baadhi ya jitihada zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta ili kuhakikisha kundi hili linapata huduma stahiki na kuboresha ustawi na maendeleo yao.
“Juhudi hizo ni pamoja na Utoaji wa huduma za afya kwa wazee, kuelimisha jamii kutambua na kuthamini mchango wa Wazee na kuendelea kutekeleza Kampeni ya “MPISHE MZEE KWANZA APATE HUDUMA”, kutoa huduma ya matunzo kwa Wazee na wasiojiweza kupitia makazi ya Wazee, ushirikishwaji wa Wazee kupitia Mabaraza ya Ushauri ya Wazee ambayo ni jukwaa muhimu linalowawezesha Wazee kuendelea kutoa mchango wao kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa letu.” amesema Naibu Mwanaidi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. James Mtatiro ametoa rai kwa wazee kuwaandaa vijana wao kuwa na uwezo wa kijimudu kimaisha mapema, ili wasiwe mizigo kwao baadaye.
“Ni muhimu wazee kuwaeleza vijana ukweli ikiwemo Taifa lilipotoka na umuhimu wa kufanya kazi na kuwajibika ili kuondokana na janga la vijana wengi kuwa tegemezi kwa wazee wao pale wanapohitimu masomo katika ngazi mbalimbali za elimu“amesema Mtatiro.
Mtatiro ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuendelea kuhudumia wazee nchini, kupitia makazi ya wazee yanayoendeshwa na Serikali kwenye mikoa mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Lameck Sendo ameiasa jamii kuwaheshimu wazee na kudumisha upendo kwani kuwanyanyasa ni mwanzo wa matatizo na laana kwa katika jamii.


No comments:
Post a Comment