Na Okuly Julius – Dodoma
Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi miongozo mipya mitano ya utoaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ikiwa ni hatua ya kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa vijana wa Kitanzania, hususan waliomaliza kidato cha sita na wanaojiandaa kujiunga na vyuo vikuu na vya kati.
Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dodoma, ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Nombo amesema dirisha la uombaji mikopo kwa njia ya mtandao litafunguliwa rasmi kuanzia Juni 15 hadi Agosti 31, 2025, hivyo kutoa muda wa kutosha kwa waombaji kusoma na kuelewa miongozo hiyo kabla ya kuanza mchakato wa maombi.
“Miongozo hii ni muhimu kwa kila mwanafunzi, mzazi na mlezi. Tunawasihi waichambue kwa makini na kufuata maelekezo yake kwa usahihi. Tumeshuhudia mara kadhaa baadhi ya waombaji kukosa mikopo si kwa sababu hawana sifa, bali kutokana na makosa ya kiufundi ambayo yangeepukika,” alisema Prof. Nombo.
Aidha, aliwataka vijana wanaotarajia kuomba mikopo kuwa na utamaduni wa mara kwa mara wa kuangalia akaunti zao za mtandaoni (SIPA) ili kufuatilia hatua za maombi yao na kufanya marekebisho pale inapobidi.
Amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imeongeza bajeti ya mikopo kutoka TZS bilioni 464 (2020/2021) hadi TZS bilioni 787 (2024/2025). Kwa mwaka wa masomo 2025/2026, serikali imetenga TZS bilioni 916.7, kiasi ambacho kinatarajiwa kufanikisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi 252,773. Kati yao, wanafunzi 88,320 ni wa mwaka wa kwanza na 164,453 ni wanaoendelea na masomo.
Aidha, wanafunzi 18,000 wa ngazi ya stashahada watapatiwa mikopo yenye thamani ya TZS bilioni 64 katika maeneo sita ya kipaumbele, yakiwemo Tiba, Elimu, Madini, Usafiri, Nishati na Kilimo.
Aidha, Prof. Nombo amesema mpango wa Samia Scholarship ulioanzishwa mwaka 2022/2023 umeendelea kuwafaidi wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi. Hadi sasa, wanafunzi 3,266 (shahada ya awali na umahiri) wamenufaika na ufadhili huo wa TZS bilioni 16.8.
Katika hatua ya kuimarisha huduma, Bodi ya Mikopo imeunganisha mifumo yake na taasisi mbalimbali kama RITA, TASAF, NECTA, TCU, NIDA, na ZHESLB, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uharaka katika utoaji wa huduma.
Aidha, kwa mwaka huu wa masomo, waombaji hawatalazimika kutuma nakala ngumu za nyaraka. Mfumo wa mtandao ulioboreshwa kupitia Mradi wa HEET utawezesha mchakato mzima kufanyika kidigitali.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Elihuruma Lema, alibainisha kuwa miongozo hiyo imekamilishwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na tayari imeidhinishwa rasmi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
"ninayo furaha kuwatangazia kuwa miongozo mitano inayozinduliwa leo imekamilika na imeidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi na kupata baraka ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na miongozo mitano inayokwenda kuzinduliwa ni Utoaji Mikopo ya Stashahada yaani Diploma, Utoaji Mikopo ya Shahada za Awali,Muongozo wa ruzuku unaojulikana kama Samia Scholarship, Muongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada ya juu ya sheria kwa vitendo, na muongozo wa utoaji mikopo kwa Shahada za uzamili na uzamivu, "
Na kuongeza kuwa “Tumefanya kazi kubwa kuhakikisha miongozo hii inaeleweka, inazingatia haki, usawa na uwazi kwa waombaji wote wenye sifa. Tunatarajia msimu huu kuwa bora zaidi,” alisema Lema.
Katika hafla hiyo, wadau wa elimu akiwemo Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Godfrey Gulagu, na Katibu Mkuu wa ZAHILFE, Ali Salum Ali, waliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji mikopo na kuahidi kuendelea kushirikiana na HESLB katika kuwaelimisha wanafunzi na kuwahamasisha kuomba kwa usahihi.
“Kama mashirika ya wanafunzi, tutaendelea kuwa kiungo kati ya serikali na vijana ili kuhakikisha kila mwenye sifa anapata fursa ya kuendelea na elimu,” alisema Gulagu.
Miongozo hiyo itapatikana kupitia tovuti rasmi za Wizara ya Elimu (www.moe.go.tz) na HESLB (www.heslb.go.tz) mara tu baada ya uzinduzi.
No comments:
Post a Comment