
Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma inakabiliwa na changamoto ya utoro uliokithiri wa wanafunzi na ukatili dhidi ya watoto, hali inayochangiwa na watoto kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali na kuacha masomo.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2025 yaliyofanyika Kijiji cha Mloda, Kata ya Mlowa Barabarani, Afisa Elimu wa kata hiyo, Amani Munna, alisema watoto wengi wanaandikishwa shule lakini hawamalizi elimu ya msingi.
“Unaweza kukuta theluthi moja ya walioandikishwa wanaacha shule kati ya darasa la pili hadi la sita. Natoa wito kwa wazazi tuwe karibu na watoto wetu, tuhakikishe wanasoma na kumaliza shule,” alisema Munna.
Munna aliongeza kuwa licha ya elimu kuwa bure kwa sera ya serikali, bado kuna mahitaji ya msingi ambayo yanapaswa kutekelezwa na wazazi kama chakula, sare na madaftari.
“Tukishindwa kuwaandaa watoto wetu kielimu, tutazalisha taifa la watu wasiojitambua ambao watapoteza rasilimali kwa wepesi. Tuwalee kwa maarifa ili tuijenge Tanzania bora,” alisisitiza.
Kwa watoto ambao hawakuandikishwa kwa wakati, Munna alisema serikali ina fursa ya elimu ya MEMKWA inayowawezesha kuingia rasmi kwenye mfumo wa elimu.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chamwino, Maua Katengu, alihimiza wazazi kuwalea watoto kwa ukaribu, kuwaonya wanapofanya makosa na kuwapa adhabu stahiki kulingana na umri wao.
“Tusiwale watoto kama mayai, lazima wafanye kazi zinazoendana na umri wao ili kuwalea katika misingi ya maadili,” alisema Katengu.
Aliongeza kuwa wazazi wahakikishe wanakuwa karibu na watoto wao, wakiwemo kuwazuia kuangalia maudhui mabaya kutoka mitandaoni, televisheni au vibanda vya video.
“Wazazi tuwape watoto muda wa kuzungumza nasi. Tusiwe watu wa mwisho kusikia mtoto kafanyiwa ukatili. Tukipanga muda wa kukaa nao, tutawasaidia kuzungumza changamoto zao kwa urahisi,” alisema.
Katengu pia alitoa tahadhari dhidi ya kuwapa watoto simu za kisasa ambazo mara nyingi huwapeleka kwenye matumizi yasiyofaa, ikiwa ni pamoja na kuangalia michezo au vipindi visivyofaa kwa umri wao.
Afisa Maendeleo wa Kata ya Mlowa Barabarani, Christina Gambo, alisema ukatili mkubwa unaanzia nyumbani kwa sababu ya wazazi kulegeza majukumu yao ya msingi ya malezi.
“Tunaamini mzazi ndiye anayemlinda mtoto, lakini kwa sasa wengi wamewachia majukumu walimu au wasaidizi wa nyumbani. Hali hii inawafanya watoto waumizwe na kufichwa madhila yao,” alionya.
Sherehe hizo ziliambatana na burudani mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, ngoma za asili, ngonjera, mashairi na maigizo yaliyobeba ujumbe wa kuelimisha kuhusu ukatili dhidi ya watoto.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila Juni 16 kwa kumbukumbu ya maandamano ya Soweto mwaka 1976, ambapo watoto walidai haki ya kupata elimu bora bila ubaguzi.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako."












No comments:
Post a Comment