WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA RASMI MASHINDANO YA UMITASHUMTA NA UMISSETA 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 9, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA RASMI MASHINDANO YA UMITASHUMTA NA UMISSETA 2025



OR-TAMISEMI, Iringa


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana kikamilifu katika kukamilisha mradi wa ujenzi wa shule 56 za kuendeleza vipaji vya michezo.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo leo, Juni 9, 2025, wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA), yaliyofanyika katika Viwanja vya Kichangani, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa.

Aidha, amezitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa ratiba za michezo zinawekwa rasmi kwenye mipango ya kila shule na kutekelezwa ipasavyo ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kushiriki michezo mara kwa mara kwa lengo la kukuza vipaji.

"Katika shule zetu tunahitaji ratiba za michezo ili vijana wetu baada ya masomo waweze kushiriki katika shughuli za michezo. Hili litasaidia kuinua vipaji na kuwaandaa kwa mashindano haya ya kitaifa," alisema Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa amevitaka vyama vya michezo vya kitaifa kupeleka wataalamu kwenye mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuwabaini wachezaji wenye vipaji maalum watakaoendelezwa kwa lengo la kuunda timu bora za taifa.

Aidha, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha walimu wa michezo wanapewa mafunzo maalum ya kisasa kuhusu sheria, mbinu na mabadiliko ya michezo, na kuwapeleka kwenye vyuo vya michezo vilivyopo nchini ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji.

Waziri Mkuu pia ameagiza Kituo cha Mafunzo cha Malia kutumika kikamilifu kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa michezo ili kusaidia kukuza vipaji vya wanafunzi katika ngazi ya shule.

Vilevile, amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa michezo hayavamiwi na shule zote za msingi na sekondari zinakuwa na viwanja kwa ajili ya michezo mbalimbali inayoshirikishwa kwenye mashindano haya.

Ameitaka TAMISEMI, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuandaa mpango mkakati wa kitaifa utakaohakikisha kila shule inakuwa na miundombinu ya michezo, ikiwemo viwanja vya riadha, ili kuimarisha ushiriki wa wanafunzi katika michezo.

Pia, amezihimiza taasisi hizo kushirikiana na wadau wa michezo, kama makampuni ya biashara yanayodhamini michezo, kuendeleza vipaji vilivyoibuliwa mashuleni kwa lengo la kuzalisha wanamichezo bora.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa vibali kwa shule binafsi na academies zinazolenga kukuza vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya awali, ili ifikapo umri wa miaka 14 vijana wawe wameimarika kitaaluma na kimwili.

Mwisho, amewataka Watanzania wote kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuwa na afya bora ambayo ndio msingi wa taifa lenye nguvu.


No comments:

Post a Comment