
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism Q1, 2025) ikisheheni takwimu za utalii duniani mpaka Mei mwaka huu, imeonesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vyema kiutalii Afrika na Duniani kwa takwimu za robo ya kwanza ya mwaka huu katika vyote; ongezeko la watalii na mapato ikilinganishwa na mwaka 2019 kabla ya Uviko.
Ongezeko la Watalii kwa Dunia na Afrika
Tanzania imeingia tatu bora ya nchi za Afrika zinazoongoza kwa ongezeko la watalii wengi ikilinganishwa na mwaka 2019 kwa kupata ongezeko la watalii kwa asilimia 50 ikitanguliwa na Moroko (asilimia 60) na Ethiopia (asilimia 52). Kwa matokeo hayo Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 bora duniani kwa ongezeko kubwa la watalii inapolinganishwa na mwaka 2019 ikitanguliwa na mataifa kama Brazil, Albania, Qatar na Saudia.
Ongezeko la Mapato Kidunia na Afrika
Katika kipengele hiki, kwa Afrika, inaonesha ripoti hiyo, Tanzania imeongoza kwa kuongeza mchango au mapato ya sekta hiyo kwa asilimia 66 ikilinganishwa na mwaka 2019 na hivyo kuwa ya kwanza Afrika (ikifuatiwa na Tunisia 62% na Moroko 49%). Kwa takwimu hizo Tanzania ni nchi ya 12 duniani ikiwa orodha moja na mataifa kama Norway, Brazil, Qatar, Saudia, Moldova n.k.
Nini Kimetokea Tanzania?
Alipoulizwa kuhusu mafanikio hayo Katibu Mkuu wa Utalii na Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassani Abbasi anasema akiwa Paris Ufaransa kikazi: “Ni mikakati. Tusingepata mafanikio haya kwa kukaa ofisini kufanya michakato miingi na kuchambua nyaraka.”
“Mhe Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoka ofisini akaenda “field” akafanya filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania; viongozi wetu wa Wizara, mabalozi wetu kote duniani, taasisi zetu na wadau wametoka kwenda kuitangaza nchi ama ana kwa ana au kushiriki maonesho makubwa. Mbegu hizo ndio zimeleta mavuno haya.
“Kwetu sisi maono ya kwenda mbele ni kuwaza mikakati zaidi ikiwemo kupitia kujitangaza kwenye ligi kubwa duniani. Ukiangalia ile ripoti utaona Qatar na Saudia wako juu ni matokeo ya mikakati pia ya vitu kama michezo na matamasha yanayofuatiliwa na nchi nyingi,” alisema Dkt. Abbasi.
Alipoulizwa matokeo hayo yanasadifu vipi uhalisia? Anajibu: “Kwanza nchi yetu imefurika watalii kila kona hapa tunavyoongea. Lakini ukiangalia takwimu zetu zinaendana na hizo za UN Tourism. Hakuna palipopungua. Taarifa ya juzi ya BoT inaonesha sekta hii imeleta Dola Bilioni 3.92 kwenye uchumi ikiwa namba moja kuleta fedha za kigeni. Makusanyo ya maduhuli kwa taasisi zote kubwa za utalii Tanapa, TFS, Tawa na Mamlaka ya Ngorongoro yamefikia viwango ambavyo havijapata kutokea tangu zianzishwe.
“Mfano katika masoko makubwa tumejitangaza sana utaona Marekani ongezeko la watalii kuja ni 41% China na India leo watalii kutoka China wameongezeka kwa asilimia 108 na kutoka India ni asilimia 75. Kona zote tunaona watalii na mapato vikiongezeka. Narudia tena na shika sana neno hili MIKAKATI.”




No comments:
Post a Comment