GST KUANZA UJENZI WA MAABARA YA KISASA GEITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 22, 2025

GST KUANZA UJENZI WA MAABARA YA KISASA GEITA




Na Mwandishi Wetu, GEITA


Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika eneo la Kanyala lililopo Halmashauri ya Mji wa Geita, mkoani Geita.

Maabara hiyo inatarajiwa kuwa ya kisasa itakayohudumia wadau wa uchimbaji na uchenjuaji madini katika mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa.

Hayo, yamebainishwa leo Julai 22, 2025 na Mtendaji Mkuu wa GST Dkt.Mussa Budeba wakati akikadhi eneo maalum la ujenzi kwa mkandarasi.

Dkt.Budeba amemtaka mkandarasi huyo ambaye ni kampuni ya Brightwave kutumia muda uliopangwa katika mkataba kukamilisha kazi hiyo ya ujenzi. Aidha, Dkt. Budeba amemtaka mkandarasi huyo kuzingatia maadili na taaluma katika kutekeleza mradi huo ili Serikali na watanzania kwa ujumla watumie miundombinu hiyo kwa muda mrefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Awali, akitoa taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa maabara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara GST, Bw. Notka Banteze amesema kuwa, maabara hiyo ndani yake itakuwa na maabara tatu ikijumuisha Sehemu ya Shughuli za Uendeshaji na Utawala na eneo la Huduma ya Chakula.

Akielezea kuhusu huduma zitakazotolewa, Banteze amefafanua kuwa ni pamoja na uchunguzi wa sampuli za miamba na madini, tafiti za uchenjuaji madini, utambuzi wa madini na uchunguzi wa sampuli za mazingira kama vile sampuli za maji na mimea.

"Maabara hii itakuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji na wachenjuaji madini, wachenjuaji madini wengi wanapoteza madini yao mengi kupitia marudio kwa kukosa uelewa wa namna bora ya kuchenjua madini kwa kuzingatia tabia za mbale". Aliongeza Banteze

Kwa mujibu wa historia ya maabara ya GST ilianzishwa mkoani Dodoma mwaka 1926 na Serikali ya kikoloni ya Uingereza (British Oversees Manegement Authority - (BOMA). Maabara hii imekuwa ikitoa huduma zake kutokea mkoani Dodoma tangu kuanzishwa kwake takribani miaka 100 iliyopita. Maabara hii itakayojengwa mkoani Geita itakuwa ya kwanza kutoa huduma za GST nje ya mkoa wa Dodoma.




No comments:

Post a Comment