Na Mwandishi wetu, Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala amewaasa watanzania kutumia sanaa na teknolojia vyema ili kuhamasisha wanawake na vijana kushiriki kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.
Mhe. Kilakala ametoa wito huo wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ushiriki wa Kiraia Kupitia Simulizi na Teknolojia ulioandaliwa na shirika la YOGE na Onastories mjini Morogoro leo Julai 22,2023.
Mdahalo huo pamoja na mengineyo ulilenga kutambua mchango mkubwa aliotoa Bibi Titi Mohamed katika harakati za kupigania uhuru.
Amesisitiza kwamba kama nchi tumepiga hatua kubwa sana katika masuala ya usawa wa kijinsia ukilinganisha na wakati nchi ilipopata uhuru ikiwemo kuwa na kiongozi wa juu ambae ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu.
Naye mwakilishi wa Onastories Bwana Francis Wairura alisema kuwa mdahalo huo in jukwaa la kukumbuka, kujifunza, na kujiuliza kama taifa tunawezaje kuendeleza urithi wa uongozi wa kweli.
“Leo tunamkumbuka Bibi Titi Mohamed — mwanamke jasiri aliyeongoza si kwa cheo bali kwa msimamo. Alivunja ukimya, alihamasisha wanawake, na alichukua hatua hata pale ilipokuwa hatari kufanya hivyo. Kwa muda mrefu, hadithi yake haijasikika kwa sauti inayostahili. Leo, tunairudisha mezani — si kama kumbukumbu tu, bali kama msukumo wa kuchochea uongozi wa sasa,” amesema Wairura.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mdahalo huo ambae pia ni mzee wa mila Mkoani Morogoro Ramadhani Rashidi amemuelezea Bibi Titi Mohamed kama mwanamke jasiri na mzalendo ambae alifanya kazi kubwa kuhamasisha wanawake kudai uhuru.
Bibi Titi Mohamed ni mwanamke shujaa ambaye alihamasisha wanawake kujiunga na TANU na kuingia kwenye harakati za kupigania uhuru ambapo pia mara kadhaa alihamasisha wanawake wa ngazi ya jamii kuchangia shughuli za chama kwa wakati ule ili kudai uhuru.
Mdahalo huo wa kitaifa umewakutanisha washiriki ambao ni viongozi katika nyanja mbalimbali kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambapo washiriki walipata fursa kuangalia na kujadili Makala maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuenzi mchango mkubwa wa Bibi Titi Mohamed katika kupigania uhuru wa Tanganyika.


No comments:
Post a Comment