JAB YAKABIDHI VITAMBULISHO VYA UANDISHI KWA WAANDISHI WALIOKIDHI VIGEZO VYA KISHERIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 24, 2025

JAB YAKABIDHI VITAMBULISHO VYA UANDISHI KWA WAANDISHI WALIOKIDHI VIGEZO VYA KISHERIA


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amemkabidhi rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Card) kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Michuzi Media Group, Bw. Muhidin Issa Michuzi, kwa niaba ya waandishi wa habari wengine waliokidhi vigezo vya kisheria vya kupatiwa vitambulisho hivyo.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za JAB jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la bodi hiyo kuhakikisha waandishi wote nchini wanatambulika kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.

Akizungumza baada ya kukabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula amempongeza Bw. Michuzi na waandishi wengine waliokwishakamilisha taratibu za kupata vitambulisho vyao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi na weledi wa tasnia ya habari nchini.

Ameeleza kuwa bado kuna waandishi wengi ambao maombi yao yamesalia katika hatua ya uhakiki kutokana na changamoto mbalimbali, hususan mapungufu katika viambatisho walivyowasilisha kwenye mfumo wa maombi.

“Mfumo wetu unakagua nyaraka zote kwa uangalifu. Tumebaini maombi mengi yameambatanishwa na nyaraka zisizosoma, nyingine zimejirudia, nyingine zina viambatisho visivyotambulika kisheria kama vile vyeti bandia, na baadhi hawajaambatanisha hata barua za utambulisho kutoka kwa waajiri wao,” alisema Kipangula.

Aidha, amewataka waandishi wa habari ambao bado hawajapata vitambulisho vyao kuhakikisha wanaingia tena kwenye akaunti zao za mtandaoni kupitia mfumo wa JAB, na kuhakiki nyaraka walizoweka, kama zinafunguka na kusomeka ipasavyo kabla ya kupiga simu kuhoji hali ya maombi yao.

Kwa mujibu wa Kipangula, Bodi itaendelea kupitia maombi kwa makundi kadri yanavyowasilishwa, huku ikiweka msisitizo kwa waandishi kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote vilivyoainishwa katika mwongozo wa kisheria uliotolewa.

Makabidhiano hayo yanakuja wakati ambapo serikali imeendelea kuhimiza weledi, uwajibikaji, na utii wa sheria miongoni mwa wanahabari nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda uhuru wa vyombo vya habari sambamba na kuhakikisha maadili ya taaluma hiyo yanazingatiwa.

No comments:

Post a Comment