
Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) umetajwa kuwa nguzo ya muhimu Wilayani Mafia katika Mkoa wa Pwani kwenye eneo la sekta ya elimu kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 20 Julai 2025 na Mbunge wa Jimbo la Mafia ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Omary Kipanga wakati akizungumza mara baada ya ziara ya jimbo akiwa Wilayani humo.
Kipanga amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano shule 4 za sekondari zimejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.717 hivyo kufanya idadi jumla ya shule za sekondari kuwa 10 ukihusisha na shule zingine 6 zilizokuwepo awali.
Kipanga amezitaja shule hizo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa shule mpya ya Kidawendui pamoja na nyumba ya mwalimu (2 in 1) iliyojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 565 katika kata ya Ndagoni, Ujenzi wa shule ya mpya ya Raphta pamoja na nyumba ya mwalimu (2 in 1) katika lata ya Kilindoni iliyojengwa kwa gharama ya shilingi 623.998, Shule mpya ya Amali Dongo iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 528.998 katika kata ya Kilindoni na Ujenzi wa shule mpya ya Jimbo iliyojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 528.998 katika kata ya Kirongwe.
Naibu Waziri Kipanga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dklt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo mpya jambo ambalo litaimarisha sekta ya elimu katika Wilaya ya Mafia na Taifa kwa ujumla wake sambamba na kuipongeza timu ya wataalamu kwa kuandika kwa weledi andiko ambalo limepelekea upatikanaji wa mradi huo.
Katika shule ya Sekondari mpya ya Jimbo inayojengwa katika kata ya Kirongwe jumla ya vyumba vya Madarasa 8 vinajengwa, Jengo 1 la Utawala, Jengo 1 la TEHAMA, Jengo 1 la Maktaba, Nyumba 1 ya Mwalimu (2 in 1), Maabara ya (Fizikia, Kemia na Baiolojia), Tenki la ardhini la maji, Kichomea taka na vyoo matundu 8.
Mhe Kipanga amesema kuwa Katika shule ya Sekondari mpya ya Raphta inayojengwa katika kata ya Kilindoni jumla ya vyumba vya Madarasa 8 vinajengwa, Jengo 1 la Utawala, Jengo 1 la TEHAMA, Jengo 1 la Maktaba, Maabara ya (Fizikia, Kemia na Baiolojia), Mnara wa Tenki la maji, Nyumba ya Mwalimu (2 in 1), Ofisi ndogo 2, Kichomea taka na vyoo matundu 16.
Katika shule Mpya ya Sekondari ya Amali inayojengwa katika kata ya Kilindoni jumla ya vyumba vya Madarasa 8 vinajengwa, Jengo 1 la Utawala, Jengo 1 la TEHAMA, Jengo 1 la Maktaba, Nyumba 1 ya mwalimu, Maabara ya (Kemia na Baiolojia), Mnara na Tenki la maji, na vyoo matundu 8.
Pia Naibu Waziri Kipanga amesema kuwa Katika shule Mpya ya Sekondari Kidawendui inayojengwa katika kata ya Ndagoni jumla ya vyumba vya Madarasa 8 vinajengwa, Jengo 1 la Utawala, Jengo 1 la TEHAMA, Jengo 1 la Maktaba, Nyumba 1 ya mwalimu (2in 1), Maabara ya (Kemia, Fizikia na Baiolojia), Mnara na Tenki la maji, na vyoo matundu 34.





No comments:
Post a Comment