
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewasili jijini Minsk, Belarus kwa ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia tarehe 21 hadi 24 Julai 2024.
Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa nchi hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alipokewa na Naibu Waziri Mkuu wa Belarus, Mhe. Viktor Karankevich na viongozi wengine waandamizi wa nchi zote mbili akiwemo Waziri wa Uwekezaji, Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick Kibuta.
Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu nchini Tanzania kuifanya nchini Belarus, inalenga kuendeleza mkakati wa Serikali zote mbili wa kuimarisha uhusiano wa uwili hususan katika sekta za kimkakati ikiwemo kilimo, elimu, afya, utalii, uwekezaji, biashara na uhaulishaji wa teknolojia.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Mkuu atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Belarus, Mhe. Alexander Turchin. Aidha, atatembelea na kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni mbalimbali za nchini Belarus kwa lengo la kuzishawishi kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Mheshimiwa Waziri Mkuu pia atashuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MoUs) kati ya Tanzania na Belarus zinazohusu kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mashauriano ya Kisiasa, kilimo, elimu na biashara.
Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Sera ya Mambo ya Nje inayolenga kukuza Doplomasia ya Uchumi.










No comments:
Post a Comment