NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefungua mafunzo ya siku tatu ya Uongozi na Usimamizi wa Shule pamoja na Utawala Bora wa Elimu kwa Maafisa Elimu kutoka mikoa yote 26 na Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara yakiwa na lengo la kuongeza ufanisi na kuimarisha usimamizi wa sekta ya elimu nchini.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Julai 29, 2025 na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu, Dkt. Emmanuel Shindika, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Bw. Atupele Mwambene ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Shindika amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa viongozi wa elimu katika ngazi za mikoa na halmashauri ili kuhakikisha usimamizi bora wa shule na kuboresha ubora wa elimu nchini.
"Tunahitaji viongozi wa elimu wenye maono, uwajibikaji na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora. Mafunzo haya yataleta mabadiliko makubwa katika usimamizi wa sekta ya elimu," amesema Dkt. Shindika.
Ameongeza kuwa serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule, ajira za walimu na utoaji wa vifaa vya kujifunzia, hivyo ni jukumu la viongozi wa elimu kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo chanya.
Amesema kuwa mpaka sasa Serikali kupitia programu ya BOOST imetoa mafunzo kwa walimu wakuu 17,794 kutoka shule zote za Msingi za Serikali kuhusu Uongozi na Usimamizi Bora wa Shule kwa kuzingatia Maeneo yote muhimu yanayohusiana na Utawala Bora katika utoaji wa Elimu.
"Pia Maafisa Elimu Kata kutoka katika Mikoa 12 ya Tanzania Bara wameshapatiwa hayo. Mafunzo haya yanayotolewa kwenu ni muendelezo wa kuwajengea uwezo Viongozi wa Elimu ili waweze kuongoza na kusimamia utoaji wa Elimu nchini kwa kuzingatia Utawala Bora". Amesema
Pamoja na hayo kupitia mafunzo hayo amewataka maafisa elimu kwenda kuonesha mabadiliko chanya katika utendaji kazi zao.
"Serikali, pamoja na washirika wa maendeleo, wametoa rasilimali na fursa za mafunzo ili kuimarisha utendaji wenu na kufikia malengo ya Program ya BOOST". Amesema
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid amesema awamu hiyo ni awamu ya kwanza ya mafunzo ya viongozi wa elimu kitaifa iliyojumuisha Maafisa Elimu Kata wa mikoa 12 kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Lindi, Mbeya, Arusha, Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mtwara na Singida.
Amesema mabadiliko makubwa yanayotarajiwa na serikali yataendelea kutokea kwani wameendelea kuwaomba na kuwasihi viongozi Maafisa Elimu wawe ndio mioyo ya kusimamia mageuzi katika sekta ya elimu.
Hata hivyo amesema kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita, ADEM ilitoa mafunzo kwa walimu wakuu 17,817 na Maafisa Elimu Kata 3,956, ambapo tathmini inaonyesha maboresho makubwa katika utendaji wao.
“Serikali inaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo viongozi hawa muhimu ili kuhakikisha mageuzi katika sekta ya elimu yanafanikiwa,” amesema.
Mafunzo ya awamu ya kwanza yamehusisha Maafisa Elimu Kata kutoka mikoa 12, huku awamu ya pili ikitarajiwa kukamilisha mafunzo kwa mikoa 14 iliyosalia.























No comments:
Post a Comment