Na. Lusungu Helela Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) tarehe 27 Agosti, 2025 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dare s Salaam.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya mkutano huo leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema pamoja na kufungua rasmi mkutano huo, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa pia ataendesha zoezi la harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Maarifa kitakachokuwa na masijala ya mfano, kumbi za mikutano pamoja na ofisi za TRAMPA kinachotarajiwa kujengwa jijini Dodoma.
Kufuatia mkutano huo wa kitaaluma, Mhe. Simbachawene ametoa wito kwa Waajiri wote kuwaruhusu Watunza kumbukumbu ili waweze kushiriki kwani ni jukwaa muhimu la kuwajengea uelewa wa majukumu wanayoyatekeleza ukizingatia kwa sasa majukumu ya kazi zao kwa zaidi ya asilimia 99 yanaendeshwa kwa mfumo wa kidijitali.
Aidha, ameongeza kuwa, ushiriki wao ni muhimu katika mkutano huo kutokana na taaluma yao hasa katika utunzaji wa siri za ofisi za umma.
Akizungumzia maandalizi ya mkutano huo, Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devotha Mrope amesema maandalizi yanakwenda vizuri huku akibainisha kuwa mwitikio wa wadhamini waliojitokeza kwa ajili ya kuhakikisha mkutano huo unafanyika umekuwa mkubwa ukilinganisha na miaka iliyopita
"Tumebahatika kupata wadhamini zaidi ya 24 na tunaamini tutawapata wengi zaidi kadiri siku zinavyokwenda" amesema Bi. Mrope
Bi. Mrope ameongeza kuwa mwitikio wa washiriki katika mkutano huo ni wa kuridhisha huku akitaja idadi ya washiriki zaidi ya 5000 watashiriki mkutano huo huku akibainisha moja ya ajenda katika mkutano huo itakuwa ni kuhamasisha wataalamu wa kada hiyo kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment