
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza leo Julia 11,2025 jijini Dodoma ,wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika ikiongozwa na kauli mbiu ya kukuza na kulinda heshima ya binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa,

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Crispin Chalamila,akizungumza leo Julai 11,2025 jijini Dodoma katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika ikiongozwa na kauli mbiu ya kukuza na kulinda heshima ya binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa
Na Okuly Julius DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ameielekeza Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Julai 11,2025 jijini Dodoma, wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika ikiongozwa na kauli mbiu ya kukuza na kulinda heshima ya binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa, ikizikumbusha taasisi zinazoratibu mapambano dhidi ya rushwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kulinda utu na haki za kila mtu ili kuimarisha utawala bora
Amesema kuwa Tanzania inajivunia hatua mbalimbali ilizochukua katika kupambana na rushwa, ikiwemo kutungwa kwa sheria, kanuni na miongozo inayolenga kukomesha vitendo hivyo.
“Serikali imeongeza bajeti, kutoa vibali vya ajira na kuruhusu ununuzi wa vifaa muhimu kwa taasisi husika ili kuongeza ufanisi wa mapambano haya,” alisema Simbachawene.
Aidha, ameeleza kuwa elimu kuhusu madhara ya rushwa imekuwa ikitolewa kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, ili kujenga jamii yenye uelewa na inayochukia rushwa.
“Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa kila mwaka. Haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na jitihada za pamoja za wananchi wote,” ameongeza.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Crispin Chalamila, amesema rushwa ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa wananchi, kwani inadhalilisha utu wa jamii.
“Kuondoa vitendo vya rushwa kutasaidia kujenga jamii yenye usawa, kuheshimiana na inayowajibika,” amesema Chalamila.
Amesisitiza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua haki ya kila raia kupata huduma bila upendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kushiriki katika vita dhidi ya rushwa.
Chalamila ameongeza kuwa TAKUKURU inaendelea kubuni mbinu mpya za kushughulikia rushwa ili kuhakikisha huduma zote za kijamii zinatolewa kwa haki bila vitendo vya rushwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), Ali Abdalla Ali, amesema maadhimisho ya kupambana na rushwa yana umuhimu mkubwa kwani hutoa fursa ya kutathmini hali halisi na kupanga mikakati mipya ya kuongeza kasi ya mapambano hayo.
“Jamii sasa inatambua kuwa rushwa ni adui wa haki, maendeleo na kwamba inachochea umaskini. Maadhimisho haya huchangia kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi na wananchi,” amesema.
Alisisitiza kuwa endapo kila mmoja atashiriki kikamilifu katika vita dhidi ya rushwa, Tanzania itakuwa nchi salama, yenye maendeleo na haki kwa wote.
Mwakilishi wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika (AUABC) , Benjamin Kapera, ameeleza kuwa kuendelea kufumbiwa macho kwa vitendo vya rushwa kumesababisha madhara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuathiri michakato ya uchaguzi barani Afrika, wagonjwa kushindwa kupata matibabu hospitalini, vijana wenye sifa kukosa haki zao, na kudhoofisha mifumo ya utoaji haki na kusisitiza umuhimu wa kuchunguza kwa kina madhara yanayotokana na vitendo vya rushwa.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Mo Ibrahim, Afrika inapoteza takribani dola bilioni 128 za Kimarekani kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa, sawa na asilimia 50 ya mapato yake ya kodi na asilimia 25 ya pato la Taifa. Kufuatia hali hiyo, Kapera amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Afrika kuchukua hatua za haraka kushughulikia tatizo la rushwa.
Pia, ametoa wito kwa Serikali za Afrika kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa usawa.







No comments:
Post a Comment