
Katika ardhi ya kusini mwa Tanzania, kwenye milima na mabonde ya Mkoa wa Ruvuma, unapatikana Mji wa Songea eneo lililobeba kumbukumbu kuu za mashujaa waliopigana kwa ujasiri dhidi ya ukoloni wa Kijerumani katika Vita ya Majimaji ya mwaka 1905 hadi 1907.
Historia inatuambia kwamba zaidi ya mashujaa 67 walinyongwa katika Mji wa Songea mwaka 1906, kwa kosa moja tu kupinga kwa ujasiri utawala wa Kijerumani.
Kati yao, mashujaa 66 walizikwa pamoja katika kaburi moja, ishara ya umoja na ujasiri usioyumba. Nduna Songea Mbano, mmoja wa viongozi waliokuwa na ushawishi mkubwa, alinyongwa peke yake na kuzikwa katika kaburi lake, ambalo hadi leo linaheshimiwa ndani ya Makumbusho ya Majimaji mjini Songea.
Makumbusho haya, yaliyofunguliwa rasmi mwaka 1980 chini ya usimamizi wa Hayati Dkt. Lawrence Gama, yameendelea kuwa kitovu cha kumbukumbu ya harakati za ukombozi.
Mwaka 2010, yalikabidhiwa rasmi kwa Shirika la Makumbusho ya Taifa na kupandishwa hadhi kuwa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii—hatua itakayoongeza mvuto wa kiutalii na kuimarisha hifadhi ya urithi huu wa kipekee.
Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ni ya aina yake nchini Tanzania, yakihifadhi silaha halisi za vita ya Majimaji, nguo, picha na ramani halisi za mapigano.
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wageni 10,000 hutembelea makumbusho hayo kila mwaka, wengi wao wakiwa ni wanafunzi, watafiti na watalii wa kimataifa wanaotaka kujifunza historia halisi ya mapambano ya wazawa wa Afrika dhidi ya ukoloni.
Lakini Songea haikujikita tu katika Vita ya Majimaji. Mkoa wa Ruvuma ulitoa mashujaa 270 waliopigana katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya 1939 hadi 1945, na miongoni mwao mashujaa hao watatu walikuwa wanawake ambao ni nadra katika simulizi nyingi za vita vya dunia.
Kando ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, sanamu za wapiganaji maarufu wa Majimaji. Sanamu hizo ni pamoja na za Mpambalyoto Soko bin Msarawani, Nduna Songea Mbano bin Luwafu, Zimamoto Gama bin Fusi, na Nduna Usangira majina yanayosikika kama mashairi ya uhuru.
Kwa wenye shauku ya kutafakari historia kwa macho, makaburi ya mashujaa 66 ni sehemu ya kivutio ambacho hutetemesha moyo wa mzalendo yeyote. Pale ndipo ilipo roho ya Songea Mbano .




No comments:
Post a Comment