
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji umeadhimisha kwa mafanikio makubwa Siku ya Kiswahili Duniani katika ukumbi wa Hoteli ya Polana Serena, jijini Maputo.
Tukio hilo muhimu limehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka makundi tofauti wakiwemo wawakilishi wa Serikali ya Msumbiji, mabalozi wa nchi mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa, wanazuoni wa lugha na tamaduni za Kiafrika, wahariri wa vyombo vya habari, pamoja na Watanzania waishio nchini Msumbiji (Diaspora).
Miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwepo ni Balozi wa Kenya nchini Msumbiji, Mhe. Philip Mundia Githiora, ambaye katika hotuba yake alieleza kuwa Kiswahili ni urithi adhimu wa Afrika Mashariki na Bara zima kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya kuimarisha uhusiano wa kijamii, kisiasa na kiutamaduni baina ya mataifa ya Afrika.
Hafla hiyo ilipambwa na burudani za kitamaduni zikiwemo ngoma ya asili ya Kimakonde, maonesho ya bidhaa mbalimbali na rasilimali za Taifa, pamoja na picha na makala za maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, na uchumi.
Akihitimisha hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, alihamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, hususan katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mhe. Balozi Hamad alisisitiza umuhimu wa kukuza na kuenzi utamaduni wa Kiswahili kama chombo cha kuunganisha jamii, kuendeleza elimu, kuimarisha diplomasia, na kuonyesha nafasi ya Tanzania kama kinara wa maendeleo ya lugha hiyo. Aidha, alieleza historia ya chimbuko la Kiswahili na mafanikio yake duniani, likiwemo ongezeko kubwa la wazungumzaji na wanaojifunza lugha hiyo katika mabara yote.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Maputo
07 Julai 2025


No comments:
Post a Comment