UGANDA YAVUTIWA MWENENDO WA BIASHARA NA MFUMO WA MASOKO TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 31, 2025

UGANDA YAVUTIWA MWENENDO WA BIASHARA NA MFUMO WA MASOKO TANZANIA


Wizara ya Madini na Fedha ya Jamhuri ya Uganda imeonesha kuvutiwa na namna Tanzania inavyoendesha shughuli za biashara ya madini, hususan mfumo wa masoko unaotumika nchini, ikilenga kuboresha mifumo yao kwa kutumia uzoefu wa Tanzania kama mfano wa mafanikio.

Hayo yamebainishwa leo Julai 31, 2025 jijini Dodoma wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Uganda uliofika katika Wizara ya Madini ya Tanzania ukiongozwa na Kamishna wa Madini wa Uganda Agnes Alabai kwa madhumuni ya kujifunza kuhusu mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini pamoja na masoko ya madini nchini Tanzania.

Pia, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwapatia mafunzo na taarifa mbalimbali zinazolenga kuboresha ufanisi wa sekta ya madini kwa kuzingatia uwazi bila kuficha taarifa yoyote.

Alabai amesema ziara hiyo imekuwa ni sehemu ya juhudi za Uganda kuimarisha sekta yake ya madini kwa kuiga mifumo yenye mafanikio kutoka mataifa jirani.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini Tanzania, Dkt. AbdulRahman Mwanga, ameukaribisha ujumbe huo kutoka Uganda na kupongeza hatua yao ya kuamua kujifunza kutoka Tanzania ambapo amesema kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya kweli ya kukuza na kuboresha sekta ya madini kwa njia ya ushirikiano wa kikanda na kubadilishana uzoefu.

“Tunafurahi sana kuona ndugu zetu kutoka Uganda wakiona umuhimu wa kujifunza kutoka kwa wenzenu hapa Tanzania. Hii ni ishara nzuri ya mshikamano wa kikanda na uelewa wa pamoja kwamba mafanikio katika sekta hii yanaweza kuimarishwa zaidi kwa kushirikiana,” amesema Dkt. Mwanga.

Aidha, Dkt. Mwanga amesema, Tanzania imefanikiwa kuanzisha na kuendesha mfumo wa masoko ya madini unaohakikisha uwazi, usalama na tija kwa pande zote zinazohusika, ikiwa ni pamoja na wachimbaji, wafanyabiashara, serikali na wanunuzi wa madini.

Naye, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini Vanance Kasiki amesema Tanzania imeendelea kuwalea na kuwainua wachimbaji wadogo ili kuweza kufanya shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa tija.

Pamoja na mambo mengine, Kisiki amesema Serikali kupitia Tume ya Madini ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini na Fedha ya Uganda kwa ajili ya kuboresha ufanisi na mifumo ya sekta ya madini ya nchini Uganda.

Kikao hicho kimehudhuriwa na maafisa mbalimbali kutoka Idara ya Madini ya Tanzania pamoja na ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Fedha ya Uganda.

Washiriki wa kikao hicho walipata fursa ya kujadiliana kwa kina juu ya mnyororo mzima wa thamani wa madini, ikiwemo usajili wa vituo vya ununuzi, udhibiti wa biashara ya madini, ukusanyaji wa mapato ya serikali na matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa biashara hiyo.

Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua katika kuboresha sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa masoko ya madini ya wazi katika mikoa mbalimbali na matumizi ya mifumo ya kidigitali ya usimamizi wa rasilimali hizo.

Ziara ya ujumbe kutoka Uganda inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini ya nchi hiyo, kwa kuimarisha mifumo ya uwazi, kuongeza mapato ya serikali na kuwezesha ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo katika soko la kimataifa la madini.







No comments:

Post a Comment