Viongozi wa klabu za michezo watakiwa kuandaa timu za SHIMIWI 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 30, 2025

Viongozi wa klabu za michezo watakiwa kuandaa timu za SHIMIWI 2025



Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Uongozi wa Shirikisho la michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa Tanzania (SHIMIWI), umewataka klabu shiriki kuandaa vyema timu zao zitakazoshiriki kwenye michezo hiyo kwa mwaka 2025 inayotarajiwa kufanyika Jijini Mwanza kuanzia tarehe 1 – 16 Septemba.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa SHIMIWI, Bw. Daniel Mwalusamba kwenye kikao cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rocky City Mall jijini Mwanza, ambapo klabu zote za wizara, idara, wakala za serikali Pamoja na ofisi za wakuu wa mikoa yote kuhakikisha wanaandaa wachezaji wao, ili waweze kuonesha michezo bora na yenye viwango.

“Hii michezo ni mikubwa na inastahili kuchezwa kwa viwango bora pia hivyo ni jukumu la kila klabu kuhakikisha wanaandaa wachezaji wao na lazima wawapime afya ili kila mmoja awe tayari kucheza kwa kuwa na afya bora, ili kuondoa majeruhi kwani wengine wanakuwa hawana mazoezi ya kutosha wanajikuta wakiumia na kupata maumivu ya muda mrefu,” amesisitiza Bw. Mwalusamba.

Halikadhalika, Bw. Mwalusamba amewataka viongozi wa klabu kukumbuka changamoto zilizotokea kwenye michezo iliyopita kwa klabu zao na kuhakikisha wanazitatua, aidha kwa kuwasilisha kwa viongozi wake au kushirikisha klabu nyingine ambazo huenda zilikuatana na changamoto kama hizo, ili waweze kuwasaidia mbinu za kuzitatua.

Amesema kila mmoja wa viongozi wa klabu wahakikishe wanafuata taratibu na kanuni lkwa kuwa kikao hiki ni moja ya majukumu waliyokasimiwa na viongozi wake mahala pa kazi, na wanapaswa kusimamia michezo mahala pa kazi vizuri, akitoa mfano kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache yamekuwa na utaratibu wa kuendesha michezo kwa watumishi wa umma mara kwa mara, ambapo amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu michezo kwa watumishi.

“Pia muwatendee haki watumishi wenzenu maana tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka mahala pa kazi kwa watumishi wanaofanya mazoezi kwa muda mrefu na kuachwa kwa makusudi, hivyo tunapaswa kuwapa fursa na tunapaswa kufanya kazi kwa kwa bidii na uadilifu kwa watumishi wenzetu waliotupa dhamana ya kuwaongoza kwenye michezo na pia kwa wananchi tunaowatumikia pia,” amesema Bw. Mwalusamba.

Hatahivyo, amewataka viongozi wa klabu kuzingatia taratibu zilizowekwa na serikali na sio kuanzisha taratibu nyingine tofauti, kwani wataonekana na kuchukuliwa hatua stahiki, kwani shirikisho limekasimiwa mamlaka ya kuendeleza michezo kwa watumishi wa umma na sio mtu mwingine nje ya shirikisho, kwani hii misingi mizuri iliyowekwa inafuatwa na kizazi cha sasa na hata cha baadaye, na sio kuvuruga utaratibu.

“Tumieni nafasi hii kuhamasishana miongoni mwenu kama viongozi kwenda kusimamia vizuri na mtakaporudi mhamasishe watumishi mahala pa kazi kushiriki michezo na mazoezi, kwani sisi watumishi wa umma tunatakiwa kuwa na afya nje ili tuwatumikie watanzania,” amesema Bw. Mwalusamba.

Bw. Mwalusamba amesema kwa mujibu wa kalenda ya shirikisho hili kabla ya kuanza kwa michezo yake, kunatanguliwa na bonanza kubwa la uzinduzi litakaloshirikisha klabu zote za shirikisho hili, ambalo litafanyika tarehe 2 Agosti, 2025 kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Bw. Alex Temba amewashukuru makatibu wakuu, wakurugenzi na watendaji wakuu kwa kuruhusu viongozi wa klabu kushiriki kwenye mkutano huu mkubwa wa maandalizi.

Hatahivyo, amesema kaulimbiu ya michezo ya mwaka huu ni “michezo huongeza tija mahala pa kazi, hima watumishi na wananchi tujitokeze kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29 kwa amani na utulivu kazi iendelee”, ambapo wanatarajia ushiriki wa klabu zaidi ya 70 zitakazotumia viwanja vya CCM Kirumba, Nyamagana, Magereza Butimba, Milongo, Nyegezi Seminari na shule ya sekondari ya Nsumba.

Bw. Temba amesema kuwa michezo hii inapelekwa kwenye kila mkoa hiyo inatoa fursa kwa wenyeji na mikoa jirani, ambapo pia wachezaji wanatoa matendo ya huruma kwa wahitaji na pia wanatembelea vivutio vya kitalii.

Nao baadhi ya washiriki walioshiriki kwenye mkutano huo wa maandalizi, kwa upande wake Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Uchukuzi, Bw. Mbura Tenga amesema kuwa utaratibu huu wa maandalizi ya michezo ni njia bora ya kutambua masuala mbalimbali ambayo yalikuwepo kwenye michezo iliyopita na kuweka sawa kwenye michezo ijayo.

Bw. Tenga amesema tayari klabu yake imeanza mazoezi kwa kanda zake nne baadaye watawachuja wachezaji na wanatarajia kubakiza 200 kutoka kwenye taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.

“Wachezaji wa klabu ya Uchukuzi wamekuwa kwenye mazoezi kwa muda wote wawapo kazini, kwani kila mwezi tumetenga kuwa na bonanza linalosimamia michezo michezo kwa kila mwezi, na tunafuatilia kwa makini ule mwongozo uliotolewa unaosema tuache tabia bwete,” amsema Bw. Tenga.

Naye Bi. Salma Hamza, ambaye ni Katibu Mkuu wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani, amesema kwa upande wao wameshiriki kwenye mkutano huu kwa lengo ya kupokea maelekezo mbalimbali kutoka kwa uongozi wa SHIMIWI.

Kwa maandalizi ya klabu yao Bi. Salma amesema wameanza mazoezi na watashiriki michezo mbalimbali, ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kuwaweka wachezaji katika afya bora.

Michezo ya SHIMIWI inashirikisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli, kuvuta Kamba, mbio za baiskeli, karata, bao, draft, darts, na riadha.





No comments:

Post a Comment