
Katika kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imegawa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili 366 kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Iringa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi pamoja na majiko hayo, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Florian Haule amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Malengo ya Mkakati huo yanafikiwa na kufanikiwa.
“Tungependa kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuamua kuibeba ajenda hii ya nishati safi ya kupikia. Pia tunaona dhamira yake ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo Mkakati huo umetuelekeza kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mhe. Rais pia ameweza kutoa fedha zilizowezesha magereza zote nchini kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia. Na leo tuko hapa kugawa mitungi ya gesi pamoja na majiko yake kwa Watumishi wa Magereza. Zote hizi zikiwa ni juhudi za Mhe. Rais kuhakikisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa vitendo” amesema Haule ambaye katika hafla hiyo pia alikuwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Stephen Mwakifwamba.
Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya ametoa rai kwa watumishi wa jeshi la magereza wote nchini kutunza miundombinu ya nishati safi ya kupikia iliyofungwa katika magereza zote nchini pamoja na kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Ackles Haule kwa niaba ya watumishi wa jeshi hilo Mkoa wa Iringa ameshkuru kwa mradi huo huku akiahidi kuwa watakuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira.
REA iliingia makubaliano na Jeshi la Magereza Septemba 13, 2024 uliolenga kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Magereza yote nchini.
Mkataba huo wenye gharama ya Shilingi Bilioni 35.23 umelenga kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya biogas, ujenzi wa miundombinu LPG, usambazaji wa mitungi ya gesi pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa magereza, usambazai wa mkaa mbadala, ununuzi wa mashine za kutengenezea mkaa mbadala na kuwajengea uwezo watumishi wa magereza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.







No comments:
Post a Comment