Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stegomena Lawrence Tax (Mb), tarehe 10 Julai 2025, amefanya ziara na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Barabara Kuu kutoka Buigiri kuelekea Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT) Kikombo mkoani Dodoma.
Mara baada ya kuwasili katika eneo la Mradi, Mhe. Waziri Tax, alipokelewa na Mkuu wa Wilaya Chamwino, Mheshimiwa Janeth Mayanja, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Dodoma, ambapo pia wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi Injinia Aloyce Mtei, Mkurugenzi wa Barabara nchini, Injinia Zuhura Amani pamoja na baadhi ya wataalam walikuwepo.
Hata hivyo baada ya kupokea taarifa fupi ya utekelezaji wa mradi na baadaye kupitishwa katika maeneo kadhaa, Waziri wa Ulinzi na JKT alibaini baadhi ya kasoro ikiwemo kuzorota kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo na akatoa maagizo ya kuona namna gani uharakishwaji unaweza kufanyika ili kuendana na muda wa kukamilishwa kwa ujenzi wa Barabara hiyo.
Aidha, ameagiza kuundwa kwa timu maalum ya mpango kazi kutoka Wizara ya Ulinzi na JKT kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi pamoja na Wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma ili kuhakikisha Ujenzi wa barabara unakamilika kwa wakati.
Naye, Mkuu wa Wilaya Chamwino Mhe Janeth Mayanja, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, amemhakikishia Waziri Tax, kuwa uongozi wa Mkoa utahakikisha unatoa ushirikiano stahiki ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kama ulivyokusudiwa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Barabara nchini, Injinia Aloyce Mtei, ametoa maelekezo kwa Wataalam wa TANROAD Mkoa Dodoma, kuandaa mpangokazi shirikishi haraka iwezekanavyo ili mradi huo uwe umekamilika.
Ujenzi wa barabara hiyo toka barabara kuu iendayo Dar el Salaam kwenda Kikombo unatarajiwa kukamilika mwezi wa septemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment