MRADI WA PEPFAR/CDC AFYA HATUA WAIMARISHA HUDUMA ZA KINGA DHIDI YA VVU MKOANI KIGOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 14, 2025

MRADI WA PEPFAR/CDC AFYA HATUA WAIMARISHA HUDUMA ZA KINGA DHIDI YA VVU MKOANI KIGOMA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Vumilia Julius Simbeye


#Kigoma yapiga hatua kubwa katika kuzuia maambukizi ya VVU Kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT) .

#Vikundi vya kina mama vina mchango mkubwa katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 

Katika kuendeleza juhudi za kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wake wa Afya Hatua, unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC), kwa kushirikiana na Serikali, limeendelea kuimarisha huduma za kinga, tiba na matunzo mkoani Kigoma. 
                                                                                                                 
Mafanikio ya kazi hii yanaonekana dhahiri katika Kituo cha Afya Kiganamo, kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu, ambapo kikundi cha akina mama wanaoishi na VVU  kinachojulikana kama Psychosocial Support Group (PSG)  kinahakikisha watoto wanaozaliwa na mama hao wanabaki salama bila maambukizi.

Faida ya kikundi cha kina mama cha PSG

Kikundi hiki hufuatilia, kuelimisha na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU pamoja na watoto wao. Hivi sasa kina jumla ya akina mama 95 — 19 wakiwa wajawazito na 76 wanaonyonyesha.
Rosemary Josephat Malela

Rosemary Josephat Malela, Mkuu wa Kitengo cha Tiba na Matunzo (CTC) katika kituo hicho, anasema:
“Tunajivunia kuona watoto waliozaliwa na mama wenye maambukizi ya VVU wakiwa salama. Hii ni matokeo ya mshikamano wa timu yetu na kina mama hawa. Jamii inapaswa kuondoa mitazamo hasi — mama anayeishi na maambukizi ya VVU anaweza kupata ujauzito na kujifungua mtoto asiye na maambukizi.”

Mikakati ya Kitaalamu na Takwimu

Kwa mujibu wa Beatrice Leonard Wilfred, Afisa Muuguzi Msaidizi, mikutano ya kila mwezi huwapa akina mama nafasi ya kujifunza mbinu salama za lishe, kuhamasishana kuhusu ufuasi wa dawa za ARV, na kushirikiana katika shughuri mbalimbali za kijamii.
Beatrice Leonard Wilfred

Amesema Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Oktoba 2024 hadi Juni 2025: wajawazito 1,058 walipimwa VVU; wane (4) waligundulika kuwa na maambukizi na kuunganishwa katika huduma ya tiba na matunzo mara moja.

"Aidha watoto 37 waliozaliwa na kina mama hawa walifanyiwa vipimo vya VVU na wote walithibitika kuwa salama (HIV negative), na Akina mama wajawazito na wanaonyonyesha 86 walipimwa kipimo cha wingi wa virusi (HVL) na 98.8% kati yao walikuwa wamefubaza VVU", ameongeza.

Ushirikiano wa Serikali na Wadau

Dkt. Moshi Kigwinya, Mganga Mfawidhi katika kituo cha afya cha Kiganamo, anabainisha kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo 8 vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa msaada wa mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika laTHPS kwa kushirikiana na Serikali.
Dkt. Moshi Kigwinya

Pius Lubavu, Msimamizi wa Huduma za mama na mtoto katika Mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua mkoani Kigoma, anasisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayeambukizwa VVU kutoka kwa mama.
Dkt. Geofrey Tarimo

Kwa upande wake, Dkt. Geofrey Tarimo, Meneja wa Mradi wa PEPFAR/Afya Hatua mkoani Kigoma, anasema kuwa katika halmashauri 9 za mkoa huu, maambukizi yamepungua kutokana na ufuasi mzuri wa dawa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Vumilia Julius Simbeye, anamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na kuwezesha ushirikiano na wadau kama THPS.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Vumilia Julius Simbeye

“Hatutacheza na afya za Watanzania. Tutaendelea kuboresha huduma za tiba na matunzo kwa kushirikiana na wadau kama THPS ili kuzuia kabisa maambukizi ya VVU,” anasema Simbeye.

Hadithi za Mama Vinara

“Mama Kinara” ni mama ambaye anaishi na VVU,aliyefubaza Virusi na anajitolea kufuatilia na kusaidia akina mama wengine katika matumizi sahihi ya dawa na ufuatiliaji wa afya ya watoto.

Consolata Amos anasema: “Baada ya kumpoteza mtoto wangu niligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na nilianza kupokea huduma ya tiba na matunzo. Kwasasa nimejaliwa kujifungua Watoto wengine wawili na wote wamezaliwa bila maambukizi. Hakuna unyanyapaa tena kuwa na VVU siyo mwisho wa maisha.”
Consolata Amos

“Nilijiunga na huduma ya tiba na matunzo mwaka 2007. Nimejifungua Watoto wawili na wote wapo salama. Sasa tunaelimishana na akina mama wenzangu na kufanya shughuli za ujasiriamali”, anaongeza Gelesia Adriano.
Gelesia Adriano

Akina mama wengine kama Naomi Petro na Leticia John wamepongeza juhudi za serikali na THPS, wakisema mafanikio haya yanaleta matumaini mapya kwa jamii.
Leticia John

Taswira ya Mkoa wa Kigoma

Utafiti wa Athari za VVU Tanzania wa mwaka 2022 (THIS 2022) unaonesha kuwa mkoa wa Kigoma una kiwango cha chini cha maambukizi ya VVU nchini ambacho kinakadiriwa kuwa 1.7%. Hali hii imechangiwa na jitihata Madhubuti za Serikali kwa kushirikiana na wadau kama THPS.

Kuhusu Shirika la THPS

THPS ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa nchini mwaka 2011 na kusajiliwa chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, likiwa na dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa urahisi.

Tangu kuanzishwa kwake, THPS inashirikiana Serikali katika kuimarisha mifumo ya afya na jamii ikikabiliana na magonjwa ya kuambukiza na magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza, afya ya uzazi, mama, watoto wachanga, vijana balehe na watoto, pamoja na kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa huduma za afya. 

Kupitia ushirikiano wa kimkakati na mbinu zinazotegemea zinazotokana na tafiti za kisayansi, THPS inatekeleza maboresho endelevu ya afya na kuunda mikakati ya afya ya umma kupitia utafiti na tathmini.

Kuhusu mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua

Mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua unatekelezwa kati ya Oktoba 2021 na Septemba 2026 katika mikoa minne: Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga, ukilenga kutoa huduma bora za kinga, tiba na matunzo ya VVU.
Meneja wa Mradi wa PEPFAR/Afya Hatua mkoani Kigoma, Dkt. Geofrey Tarimo.
Msimamizi wa Huduma za mama na mtoto katika Mradi wa PEPFAR/CDC Afya Hatua mkoani Kigoma, Pius Lubavu.

No comments:

Post a Comment