MWALIM WA CHAUMMA ACHUKUA FOMU KUGOMBEA URAIS , AAHIDI MABADILIKO MAKUBWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 12, 2025

MWALIM WA CHAUMMA ACHUKUA FOMU KUGOMBEA URAIS , AAHIDI MABADILIKO MAKUBWA




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amejitokeza rasmi kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, Agosti 12, 2025, akiahidi kuleta mageuzi makubwa kwa Watanzania endapo atapata ridhaa ya kuongoza taifa.

Akiwa ameambatana na viongozi na wanachama wa chama hicho kutoka ngazi mbalimbali, Mwalimu alisema hatua hiyo ni mwanzo wa safari muhimu ya kisiasa kwa yeye binafsi na kwa CHAUMMA kwa ujumla.

“Tunakwenda kuibadilisha historia. Kipaumbele chetu ni kuinua sauti ya wananchi na kuleta mageuzi. Kampeni zetu rasmi tutazindua Zanzibar, tukiomba ridhaa ya Watanzania wote kutuamini ili tuwatumikie,” alisema Mwalimu.

Amesema hofu au vikwazo vyovyote vitakavyojitokeza haviwezi kukwamisha azma yao, akisisitiza kuwa yeye na mgombea mwenza wake ni viongozi wasafi kimaadili na kiutendaji.

“Kama kiongozi msafi sina deni kwa mtu yeyote. Mimi na mgombea mwenza tuna rekodi safi na tunatoa fikra safi bila mawaa yoyote,” alisisitiza.

Kuhusu mageuzi wanayokusudia, Mwalimu alisema msingi wake utaanzia kwenye Katiba, ili kuanzisha serikali inayolenga haki za watu na kuwahakikishia uhuru wa kweli bila ubaguzi.

Akiwashukuru wananchi wa Dodoma kwa mapokezi makubwa, alisema anaimani maeneo mengine ya nchi yataonesha mshikamano sawa, akiahidi kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha Tanzania inapata mustakabali bora.

“Safari hii si ya mtu mmoja, bali ni ya chama chote na Watanzania wote wanaotaka kuona maendeleo na mabadiliko chanya,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea mwenza Devota Minja aliwataka Watanzania kuendelea kuwaamini wanawake na kutozipuuza nafasi zao katika siasa na maendeleo ya taifa.

Amesema wanawake ni nguzo muhimu katika kusukuma ajenda za maendeleo, hususan kwenye sekta za afya, elimu, maji, na masuala ya afya ya uzazi.

“Watanzania wanatambua uwezo wa wanawake katika uongozi. Tumeona jinsi wanawake wanavyoweza kusaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye masuala yanayogusa maisha ya kila siku. Mimi na mgombea mwenza tutashirikiana kwa dhati kusukuma gurudumu hili kwa maendeleo ya taifa,” alisema Minja.















No comments:

Post a Comment