Mgombea nafasi ya kiti cha Urais kupitia tiketi ya Chama Makini, Coaster Kibonde, amesema endapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kila Mtanzania atapatiwa ekari tano pamoja na trekta kwa ajili ya kuendeleza kilimo, ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kibonde, aliyewasili majira ya saa 09:09 Asubuhi katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) akiwa na mgombea mwenza na wanachama wenzake wa chama hicho, amesema kilimo ni moja ya vipaumbele vitatu vya chama chake, vingine vikiwa ni elimu na afya.
Ameeleza kuwa katika elimu, kila Mtanzania atapaswa kusoma kwani kuinyima jamii elimu ni kuikwamisha kwenye maendeleo ya kiuchumi. Kuhusu afya, amesema wataanzisha bima itakayojulikana kama Bima Makini, ambayo kila mmoja atapaswa kuwa nayo ili kuhakikisha anapata matibabu pindi anapokumbwa na changamoto za kiafya.
Leo, vyama vitatu vya siasa vinatarajiwa kuchukua fomu za kugombea nafasi ya kiti cha Urais katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Njedengwa jijini hapa.
No comments:
Post a Comment