RC KILIMANJARO AVUTIWA NA JITIHADA ZA EWURA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 8, 2025

RC KILIMANJARO AVUTIWA NA JITIHADA ZA EWURA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA



MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu,akizungumza leo, Agosti 8, 2025, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika Viwanja vya Themi – Njiro, jijini Arusha.


Na Mwandishi Wetu, Arusha


MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa juhudi zake za kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan gesi ya mitungi (LPG), kama njia ya kuboresha afya ya jamii na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza leo, Agosti 8, 2025, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika Viwanja vya Themi – Njiro, jijini Arusha, Mhe. Babu amesema kuwa juhudi hizo za EWURA zina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.

“Ni muhimu wananchi waelewe faida za kutumia nishati safi ya kupikia. Mbali na kupunguza athari za kiafya zitokanazo na moshi wa kuni na mkaa, pia tunalinda mazingira yetu dhidi ya uharibifu,” amesema Mhe. Babu.

Katika maonesho hayo, EWURA kupitia ofisi yake ya Kanda ya Kaskazini, ilishiriki kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama na sahihi ya gesi ya mitungi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa watumiaji na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kuelekea matumizi ya nishati mbadala.

Maafisa wa EWURA walieleza kuwa elimu hiyo inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanafahamu jinsi ya kutumia vifaa vya LPG kwa usahihi, hatua za kuchukua ili kuepuka ajali, pamoja na kuzingatia ubora wa bidhaa wanazonunua.

Ushiriki wa EWURA katika maadhimisho ya Nanenane mwaka huu unaendelea kuonyesha dhamira ya mamlaka hiyo katika kushirikiana na wananchi na wadau wa sekta mbalimbali, kwa lengo la kuleta maendeleo jumuishi na kuimarisha ustawi wa jamii kupitia huduma bora za nishati.

No comments:

Post a Comment