
NA.MWANDISHI WETU – DODOMA
Serikali imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II), hususan katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.
Akizungumza katika kikao kazi cha waratibu wa programu hiyo kilichofanyika leo Agosti 27, 2025 jijini Dodoma, Mratibu wa Taifa wa ASDP II kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Salim Nandonde, alisema sekta binafsi ni nguzo muhimu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo na mifumo ya chakula nchini.
“Uratibu wa ASDP II unaoratibiwa katika ngazi ya taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na OR-TAMISEMI katika ngazi za mikoa na halmashauri, unalenga kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu, hasa kwenye kuongeza thamani katika mazao na mifumo ya chakula ili kuongeza tija na ushindani,” alisema Dkt. Nandonde.
Akiainisha maeneo ya utekelezaji wa programu hiyo, Dkt. Nandonde alitaja dhana ya mifumo ya chakula inayohusisha hatua zote kuanzia uzalishaji, usambazaji, uhifadhi, usalama wa chakula na lishe, kilimo biashara, pamoja na mifumo endelevu inayohimili changamoto za dharura.
Aidha, alibainisha kuwa kikao hicho pia kinatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau kuhusu namna ASDP II inavyoweza kufungua milango ya fursa za uwekezaji na ushiriki mpana wa sekta binafsi.




No comments:
Post a Comment