SIASA ZANGU NI ZA MAENDELEO - MHE MCHENGERWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 1, 2025

SIASA ZANGU NI ZA MAENDELEO - MHE MCHENGERWA




Na Mwandishi Wetu - Rufiji.


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Rufiji ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo anayemaliza muda wake Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema siasa anazozifanya ni za maendeleo, ambazo dhamira yake ni kuwakomboa wananchi wa Rufiji kwa kuwaimarisha kiuchumi pamoja na kuwajengea miundombinu bora ya afya, elimu na barabara.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati akiomba kura kwa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi wa Kata za Mkongo, Ngorongo, Kipugira na Mwasemi zilizopo katika Jimbo la Rufiji.

“Siasa zangu ni siasa za maendeleo, nimedhamiria kuwakomboa ndio maana nikilala na kuamka nawaza maendeleo ya Rujiji hivyo ninaomba kura zenu wanarufiji kwani sitowaangusha,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewathibitishia wananchi wa Rufiji kuwa, kupitia Miradi ya Benki ya Dunia kiasi cha bilioni 30 zitatumika kujenga barabara kwa kiwango cha lami, stendi za kisasa na masoko ya kisasa.

“Moyoni mwangu ipo Rufiji hivyo mapenzi yangu kwa Rufiji hayajifichi, ninawaomba wanarufiji wenzangu mniamini kwani sitowasaliti,” Mhe. Mchengerwa ameeleza bayana.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wa Rufiji waendelee kumuamini kwani amejenga shule za Sekondari 22 kutoka 4 alizozikuta, amejenga shule za msingi 63 kutoka 20 alizozikuta, amejenga vituo vya afya 9 kutoka 3 vilivyokuwepo hivyo anaamini miaka 5 ijayo hakutakuwa na kata isiyo na kituo cha afya.

Mhe. Mchengerwa amehimiza kuwa, yuko tayari kuendeleza dhana yake ya mapinduzi ya fikra ya miaka 10 ya uongozi wake akiwa Mbunge wa Jimbo la Rufiji, hivyo amewaomba wananchi wa Rufiji wamuunge mkono kwa kumpa kura nyingi ili aendelee kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.

Mhe. Mchengerwa amepata fursa ya kuomba kura kwa wajumbe wa Kata za Mkongo, Ngorongo, Kipugira na Mwasemi ikiwa ni sehemu ya Mchakato wa Kura za Maoni ndani CCM, ambapo aliambatana na wagombea wenzie wanne ambao ni Salma Ponga, Hamisa Kisoma na Seleman Mhekela ambao Julai 28, 2025 waliteuliwa na Kamati Kuu ya CCM.





No comments:

Post a Comment