
OR -TAMISEMI,Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Vijiji na Miji Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Mkuki Hante, leo (Agosti 28, 2025), amezindua rasmi Mjadala wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wenye lengo la kufungua miradi ya uwekezaji kupitia ushirikiano kati ya Halmashauri na sekta binafsi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais TAMISEMI Adolf Ndunguru, Dkt. Hante amesema Serikali imeandaa Rasimu ya Mpango wa Msaada wa Utekelezaji wa Miradi ya Halmashauri ili kuongeza ufanisi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kipaumbele katika Halmashauri za Mwanza, Ilemela na Tanga.
“Tumeona changamoto nyingi katika maandalizi na utekelezaji wa miradi. Kupitia mpango huu tunataka kujenga uwezo wa Halmashauri, kuvutia wawekezaji na kuhakikisha miradi inatekelezeka kwa vitendo kupitia PPPs na ushirikiano mwingine wa sekta binafsi,” amesema
Mjadala huo uliofanyika jijini Dar es Salaam,ulihusisha viongozi wa serikali za mitaa, mabenki, taasisi za kifedha, mashirika ya hifadhi ya jamii, wawekezaji na washirika wa maendeleo. Washiriki walipata fursa ya kujadili miradi ya kipaumbele na kutoa ushauri juu ya namna ya kushirikiana katika utekelezaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Hante, Serikali imeridhia kuanza na vipaumbele vitatu hadi vinne vya awali, ikiwemo mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kujengea uwezo timu za Halmashauri.
“Mjadala huu si jukwaa la maneno pekee, bali ni daraja la kuunganisha nguvu kati ya sekta ya umma na binafsi kwa maendeleo ya wananchi,” amesisitiza.





No comments:
Post a Comment