
CPA Marwa ameyasema hayo Agosti 24, 2025, katika banda la TTCL kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kinachoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC jijini Arusha, kilichofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango.
Amesema TTCL ndiyo taasisi pekee nchini inayomiliki Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku Serikali ikiendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa ili kufanikisha ajenda ya uchumi wa kidijitali.
“Hatua hii inalenga kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yenye changamoto ambazo kwa kawaida watoa huduma binafsi hawawezi kufika kutokana na kutolipa kibiashara,” alisema CPA Marwa.
Aidha, amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu miezi sita iliyopita, zaidi ya minara 100 imekwishajengwa, na matarajio ni kwamba ifikapo Juni 2026, minara yote 620 iliyopangwa kwa mwaka huu itakuwa imekamilika.
Ameongeza kuwa TTCL imejipanga kuhakikisha minara hiyo inaunganishwa moja kwa moja na Mkongo wa Taifa, ili wananchi wapate huduma za intaneti yenye kasi na uhakika.
Vilevile, CPA Marwa amekumbusha kuwa mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mkakati wa kidijitali unaolenga kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka msisitizo mkubwa katika eneo hilo.
Mbali na Mkongo wa Taifa, TTCL pia ina kituo cha Data Center kinachowezesha mifumo ya kidijitali nchini kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Uwekezaji huu unaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya teknolojia, huku wananchi wakinufaika na huduma bora za mawasiliano, ikiwemo intaneti ya kasi kubwa inayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.










No comments:
Post a Comment