
Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Kitengo cha Msaada wa Kisheria Mama Samia Legal Aid Campaign imeendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Huduma hizo zinalenga kusaidia wananchi kupata haki zao kwa njia ya sheria, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kisheria, uandishi wa nyaraka kama wosia na mikataba, pamoja na elimu ya haki na wajibu wa kisheria kwa wananchi.

Mmoja wa wananchi walionufaika na huduma hiyo ni Abdallah Chuma, mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amesema alihangaika kwa muda mrefu katika ofisi mbalimbali za serikali kutafuta suluhisho la mgogoro wa umiliki wa nyumba ya familia yao, bila mafanikio.
“Nimekuja hapa na nimepata msaada wa haraka. Tatizo langu ni kubwa. Baba yangu mdogo alinunua nyumba kupitia mnada wa mahakama, lakini hakufanikisha kuhamisha umiliki kwenda kwa jina lake. Mtu mwingine alijimilikisha nyumba hiyo na baadaye akaamua kuiuza. Ilinisikitisha sana, lakini sasa nimepata mwanga wa nini cha kufanya kisheria,” amesema Abdallah.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka wizara ya katiba na sheria Marco Lucas amethibitisha Kumhudumia Chuma huku akisisitiza kuwa huduma hizi zitaendelea kutolewa kwa wananchi wote walioko kwenye viwanja hivyo, na kwamba lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki mbele ya sheria bila kujali hali ya kiuchumi.


No comments:
Post a Comment