
Mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa wananchi wanahitaji huduma na maendeleo yanayotokana na utekelezaji wa mipango thabiti na sio kwa maneno yasiyotekelezeka.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 11, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Butinzya wilayani Bukombe mkoani Geita.
“ Hawa wananchi wanataka huduma hawataki maneno kazi yangu ni kusogeza huduma kwa watu, nataka mgombea udiwani Mathias hii Zahanati ya Butinzya ikamilike katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kuchaguliwa,” amesema Dkt. Biteko
Amesisitiza “Tunahitaji ukamilishaji wa haraka nimenunua vifaa, nataka tumalize hapa tuangalie kitu kingine. Tuna mpango wa kujenga vituo vya afya 59 katika Wilaya Bukombe,”
Ameendelea kusema wamejenga barabara ya lami na wanataka wananchi wa Kata hiyo wapite kwenye barabara hiyo za lami kwenda Ushirombo na maeneo mengine, umeme ufike kwenye vitongoji vyote huku akisisitiza kuwa mipango ya maendeleo hailetwi kwa kusema sana na kuwa CCM wanatekeleza mipango hiyo kwa vitendo.
Fauka ya hayo, amesema Rais Samia ametoa fursa kwa wananchi kufanya maendeleo Bukombe akitolea mfano kuruhusu wananchi kuchimba madini katika Pori la Kigosi.
“ Mambo yanaenda kwa sababu Rais Samia anatupenda na sasa utaona maendeleo Bukombe kwa sababu ametoa fursa ili watu wapate maendeleo, niwaombe Oktoba 29 mwaka huu tumpigie kura nyingi, watu wote tujitokeze kupiga kura,” ameongeza Dkt. Biteko.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Kihanja Lutonja amewaomba wananchi wa Kata hiyo kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani kwa kuwa CCM ina dira inayotekelezeka na hivyo wakiamini chama hicho ili kiendelee kushika dola na kutumiza matarajio yao na ya Watanzania kwa ujumla.
Mgombea wa Udiwani Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuhakikisha kuwa katika uongozi wake miradi ya maendeleo imetekelezwa katika Kata hiyo ikiwemo ya afya na barabara.
Aidha, ameahidi kuwa akichaguliwa atawaletea maendeleo wananchi wa Kata hiyo.



No comments:
Post a Comment