
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Septemba 11 anatarajiwa kuendelea na kampeni zake kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwenye Wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.
Kampeni hizo zinaendelea kwenye Kanda hiyo ya Kati, ikiwa ni siku ya pili ya kampeni zake mkoani Tabora, ambapo jana Jumatano akiwa Igunga pamoja na mambo mengine, aliahidi kujenga kituo cha mabasi cha kisasa na soko la kisasa ili kuongeza wigo wa biashara na kuvutia uwekezaji, akiahidi pia kujenga barabara za lami zinazopita maeneo ya uzalishaji wa mpunga, mbaazi, dengu na choroko na uchimbaji wa madini ili kuongeza kasi ya kukuza uchumi.
Dkt. Samia ameahidi pia kujenga kituo cha kupokea na kupooza umeme kwa kuwa Igunga ina mahitaji makubwa ya nishati ya umeme hasa ikizingatiwa kuwa serikali yake itaanzisha konganin ya viwanda kwaajili ya kuongeza thamani ya mazao pamoja na kuja na njia sahihi ya kudhibiti wanyamapori waharibifu ambao wamekuwa kero kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi.
Katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2025/30, Wameahidi kukamilisha ujenzj wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum kwenye shule ya msingi Kaliua, Ukamilishaji wa maabara ya shule ya sekondari Isike, ujenzi wa bwawa na skimu ya Kona 4, Igombe, Mnange, Limbula na Igwisi huku Iyui kukiahidiwa ujenzi wa zahanati mpya kwenye Vijiji vya Hiari ya Moyo, Mhulidede, Mdalaigwe, Kalemela, Nzubuka, Mwamabondo, Bukala, Mhalule, Itobela na Kigwanhona.
CCM pia imepanga kupanua mradi wa maji wa Ziwa Viktoria, ujenzi wa bwawa na skimu ya Majengo, Mbola, Mwakashindiye, Igalula, Mwamabondo, Loya, Miswaki, Shitage na Goweko pamoja na ujenzi wa barabara ya Kilomita mbili katika makao makuu ya Wilaya ya Uyui kwa kiwango cha lami, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe katika barabara za Kigwa- Itundaukulu (Km10), Magiri- Kalemela-Itobela (Km12), Ndono- Ufumula (Km30), Isuli- Miyenze (Km20), Mabeshi- Loya (Km30), Tura- Mwamlela- Lutona (Km25) na Keza- Igombe.
Kwa Urambo Ilani ya CCM imepanga kujenga Zahanati 15 na kituo cha afya, ujenzi wa vyumba vya madarasa 350 shule za msingi na sekondari, ujenzi wa shule ya msingi yenye mtaala wa kiingereza katika Wilaya ya Urambo, ujenzi wa shule mpya 12 za msingi na sekondari, ujenzi wa somo la mazao, Pamoja na kuendeleza ujenzi wa vibanda kwenye stendi kuu ya mabasi na ujenzi wa soko jipya mtaa wa St. Vincent.
No comments:
Post a Comment