
Na Sixmund Begashe, Iringa
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amezitaka taasisi za uhifadhi nchini, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuongeza kasi ya kuhamasisha utalii wa ndani ili Watanzania waweze kunufaika moja kwa moja na matokeo chanya ya uhifadhi wa rasilimali za utalii.
Dkt. Kijaji ametoa wito huo wakati wa kikao chake na menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na viongozi wakuu wa TANAPA na TAWA, kilicholenga kutathmini utekelezaji wa mikakati ya kukuza sekta ya utalii nchini.
Amesema kasi ya kuchechemua utalii na kuimarisha uhifadhi endelevu Kusini mwa Tanzania, inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo.

Amebainisha kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa vivutio vya asili, hususan katika ukanda wa kusini, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, malazi ya watalii, pamoja na kuwawezesha kiuchumi wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi, hatua inayolenga kuvutia zaidi watalii wa ndani na nje pamoja na wawekezaji.
Akiwa ameambatana na Mhe. Hamad Hassan Chande, Dkt. Kijaji amezisisitiza TANAPA na TAWA kuhakikisha zinaimarisha mikutano ya ujirani mwema na nchi jirani, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuitangaza Tanzania kama kivutio bora cha utalii, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030.
“Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatutaka tufikie watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030. Sisi kama wasimamizi wa sekta, tunapaswa kumpatia Mhe. Rais wetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye Mhifadhi na Muongoza Watalii namba moja nchini, zawadi ya kuvuka malengo haya. Mhe. Rais tayari ameshaamua kuinua sekta ya utalii; sisi hatutakiwi kushindwa hata kidogo. Tupige kazi,” amesema Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amemhakikishia Waziri Kijaji kuwa ofisi yake itahakikisha maelekezo na maagizo yote yanatekelezwa kikamilifu kwa lengo la kufanikisha malengo ya sekta ya utalii nchini.




No comments:
Post a Comment