
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba amesisitiza mwelekeo na mkakati wa Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa hapa nchini yanaongezewa thamani ndani ya nchi, ikiwa ni nguzo muhimu ya kuongeza Mapato ya Taifa, Mchango wa Sekta katika Pato la Taifa (GDP), ajira na maendeleo ya mnyororo mzima wa thamani katika Sekta ya Madini.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 17, 2025 wakati akizungumza na Watumishi wa Tume ya Madini – Mkoa wa Kimadini Arusha pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha.

Mhandisi Samamba amesema Serikali ina matarajio makubwa kupitia Sekta ya Madini, hususan katika kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa, hatua itakayoongeza mapato, kukuza viwanda vya ndani na kutoa fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.
“Maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni lazima tuhakikishe value addition na beneficiation vinafanyika ndani ya nchi.
Huu ndio mwelekeo wa Serikali katika kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia kikamilifu uchumi wa Taifa, hii ni moja ya rasilimali tulizojaaliwa kwa wingi, lazima yachangie kukuza uchumi wetu kama taifa” amesisitiza Samamba.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ameeleza kuwa wachimbaji wadogo wataendelea kupewa kipaumbele, akibainisha kuwa kundi hilo ni moja ya mihimili muhimu wa Sekta ya Madini na lina mchango mkubwa katika uzalishaji na ukusanyaji wa maduhuli.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wachimbaji wadogo kuongeza tija, ufanisi na mchango wao katika uchumi.
Akiwahimiza Watumishi wa Tume ya Madini na TGC, Eng. Samamba amesisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja, akiwataka kuzingatia weledi, maadili ya utumishi wa umma na kuachana kabisa na vitendo vya rushwa.
Vilevile amekemea matumizi ya lugha zisizoridhisha kwa wateja, akisisitiza kuwa lugha nzuri ni sehemu ya heshima, uwajibikaji na taswira chanya ya Serikali.
“Huduma bora kwa wateja, kuepuka rushwa na matumizi ya lugha inayojenga heshima ni msingi wa mafanikio ya Taasisi zetu na sekta kwa ujumla,” ameongeza Eng. Samamba.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uzalendo, ili Sekta ya Madini iendelee kuwa kichocheo cha maendeleo endelevu na uchumi jumuishi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mratibu wa TGC Mhandisi Ally Maganga ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) umefikia asilimia 10, akibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mafunzo, utafiti na uongezaji thamani wa madini ya vito nchini.
Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha Francis Mihayo amesema kuwa mkoa wa Arusha unaendelea kuchukua hatua madhubuti kutekeleza maelekezo ya Serikali hususan kupitia usimamizi makini wa shughuli za uchimbaji, uchakataji na biashara ya madini.
Amesema Ofisi ya Afisa Madini Mkazi itaendelea kushirikiana kwa karibu na wachimbaji wadogo, wawekezaji na taasisi za Serikali ikiwemo Tume ya Madini na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), ili kuhakikisha mazingira rafiki ya uwekezaji, ufuataji wa sheria na kanuni, pamoja na kukuza mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya kiuchumi ya mkoa na Taifa kwa ujumla.






No comments:
Post a Comment