DODOMA JIJI YATOA ONYO: WADAIWA VIWANJA MTUMBA, KIKOMBO WAPEWA SIKU 21 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 29, 2025

DODOMA JIJI YATOA ONYO: WADAIWA VIWANJA MTUMBA, KIKOMBO WAPEWA SIKU 21




Na Carlos Claudio, Dodoma.


Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekamilisha zoezi la awali la uhakiki wa wadaiwa wa viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone II, Mtumba Zone III na Kikombo, viwanja vyenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 55.4.

Hatua hiyo imelenga kuimarisha uwazi, haki na uwajibikaji katika usimamizi wa ardhi ya umma pamoja na kuhakikisha Halmashauri inapata mapato halali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 29, 2025 jijini Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe, ambaye amesema zoezi hilo lililenga kuwatambua watu binafsi, taasisi na kampuni ambazo bado hazijakamilisha malipo ya viwanja walivyoomba na kupatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Amefafanua kuwa katika eneo la Mtumba Zone II kuna jumla ya viwanja 1,915 vyenye thamani ya shilingi bilioni 28.8, Mtumba Zone III kuna viwanja 2,594 vyenye thamani ya shilingi bilioni 20.6, huku eneo la Kikombo likiwa na viwanja 2,051 vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.9. Kwa ujumla, viwanja vyote vilivyohakikiwa vina thamani ya shilingi bilioni 55.4.

Kwa mujibu wa Gondwe, matokeo ya uhakiki huo yamebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wadaiwa ambao hawajalipa kabisa au wamelipa sehemu ya gharama za viwanja hivyo, hali ambayo imeisababishia Halmashauri ya Jiji la Dodoma usumbufu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

“Kutokukamilika kwa malipo ya viwanja kumeathiri utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu ikiwemo ufunguzi wa barabara, usambazaji wa umeme, maji pamoja na huduma nyingine muhimu katika maeneo yanayotekelezwa miradi ya upimaji wa ardhi,” amesema Gondwe.


Ameongeza kuwa hali hiyo pia imeathiri maeneo mengine ya utoaji wa huduma za kijamii, kwani fedha zinazotokana na mauzo ya viwanja ni sehemu ya mapato yanayotarajiwa kutekeleza Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kutokana na hali hiyo, Menejimenti ya Halmashauri imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa na kutangaza orodha rasmi ya awali ya wadaiwa wa malipo ya viwanja.

Orodha hiyo inaonesha majina ya wadaiwa, namba za viwanja pamoja na vitalu husika, ikiwa ni jitihada za kuwasaidia wadaiwa kukumbuka na kuhakiki taarifa za viwanja vyao.

Vilevile, Halmashauri imetoa notisi ya siku 21 kwa wadaiwa wote kuhakikisha wanalipa madeni yao, au kukamilisha malipo yaliyobaki kwa wale waliolipa sehemu ya deni, kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria na kiutawala.


Gondwe amesisitiza kuwa viwanja vyote ambavyo malipo yake hayatakuwa yamekamilika baada ya kumalizika kwa siku 21 za notisi vitarejeshwa sokoni rasmi kuanzia Desemba 30, 2025, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa ardhi.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa wito kwa wadaiwa wote wa viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone II, Mtumba Zone III na Kikombo kujitokeza kwa wakati na kukamilisha malipo yao ndani ya muda uliotolewa ili kuepuka usumbufu na kupoteza haki zao za umiliki wa viwanja husika.

Aidha, wale wote ambao majina yao yamejitokeza katika orodha ya wadaiwa lakini tayari wameshakamilisha malipo ya viwanja wanatakiwa kufika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakiwa na nyaraka halisi (original) za uthibitisho wa malipo ili kufanyiwa uhakiki na marekebisho stahiki.

Orodha kamili ya awali ya wadaiwa inapatikana katika Gazeti la Mwananchi la tarehe 30 Desemba, 2025, tovuti ya Halmashauri www.dodomacc.go.tz pamoja na mitandao ya kijamii ya Halmashauri kupitia Instagram @dodomacc_tz na Facebook ukurasa wa Dodoma Council.

Kwa maelezo zaidi, wananchi wanashauriwa kufika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ofisi za iliyokuwa Manispaa ya zamani, Duka la kuuzia viwanja Namba 03, au kuwasiliana kupitia simu namba 0754 551 694 au barua pepe cd@dodomacc.go.tz.





No comments:

Post a Comment