KONGANI YA VIWANDA KAHAMA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA UZALISHAJI BIDHAA ZA MGODINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 21, 2025

KONGANI YA VIWANDA KAHAMA KUIFANYA TANZANIA KUWA KITOVU CHA UZALISHAJI BIDHAA ZA MGODINI



Na Mwandishi Wetu, Shinyanga


Kufuatia kuhitimishwa kwa shughuli za uchimbaji katika eneo la Buzwagi, Serikali imeweka mkakati na kutenga eneo hilo kwa ajili ya viwanda hususan vya uzalishaji wa bidhaa na huduma za mgodini na kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa na huduma kusini mwa jangwa la Sahara.

Hayo yameelezwa leo Desemba 21, 2025 na Waziri wa Madini, *Mh. Anthony Mavunde* alipotembelea na kukagua eneo hilo la kongani ya viwanda Buzwagi, lililopo Kahama Mkoani Shinyanga.

Waziri Mavunde amesema kuwa, Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* anataka kuona eneo la Buzwagi linabadilishwa na kuwa kitovu cha uchumi wa viwanda nchini.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, zaidi ya viwanda 30 vitajengwa katika sekta mbalimbali ikiwamo nishati, Elimu , uzalishaji bidhaa za migodini, bidhaa za kuchakata madini, na bidhaa zingine zinazotumika kwenye sekta ya madini ikiwemo vipuli vya viwandani.

Pia, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Mgodi wa Buzwagi ulikuwa ni chachu ya maendeleo na uchumi wa Kahama, hivyo kufungwa kwake kungeweza kuyumbisha mapato ya Wilaya, hivyo kuanzishwa kwa Kongani hiyo kunakwenda kunufaisha wananchi wa Kahama na Taifa kwa ujumla kupitia ajira na shughuli zinginezo.

"Zaidi ya wawekezaji 30 wameonesha nia ya kuanzisha viwanda katika eneo la Buzwagi, na tayari mwekezaji mmoja aitwaye East Africa Conveyors Supplies ameanza kuzalisha bidhaa zinazotumika migodini. Hii ni hatua muhimu sana kwenye sekta ya madini kwani awali bidhaa hizo zilikuwa zikiagizwa Nje ya Nchi yetu" alisisitiza Mhe. Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alieleza kuwa Kampuni ya Tembo Nickel itajenga kiwanda cha kuongeza thamani madini ya metali (*Multi-Metal Refinery Facility*) katika eneo hilo ambacho kitakuwa ni moja ya viwanda vikubwa Barani Afrika ambacho kitatumia teknolojia ya kisasa ya 𝙃𝙮𝙙𝙧𝙤𝙢𝙚𝙩 ambayo inatumia umeme kidogo badala ya kuyeyusha kwa joto kali.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuweka mikakati mizuri ya kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga ambapo kupitia uwekezaji huu fursa mbalimbali zitajitokeza na kuchochea ukuaji wa uchumi kuanzia ngazi ya mkoa mpaka taifa.

Mhita ameongeza kuwa, eneo la Buzwagi tayari lina miundombinu mizuri , nishati ya umeme na vyanzo vya maji hivyo ni fursa kubwa kwa watanzania kuja kuwekeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na maeneo maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Bw. Gilead Teri ameeleza kuwa,Serikali, kwa kushirikiana na wawekezaji, imeanzisha Buzwagi Special Economic Zone ambayo ina mpango wa kuwa kitovu cha uzalishaji, usindikaji na usambazaji wa bidhaa za mgodi kwa soko la Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

Teri ameongeza kuwa, uwekezaji umeanza kuvutia makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi, na baadhi yao tayari wametia saini kuanzisha shughuli za uzalishaji ndani ya Buzwagi SEZ, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa wafanyakazi wa mitaa na kuongeza pato la taifa.

Wakizungumza katika ziara hiyo wabunge wa Kahama Mjini na Msalala Mh. Benjamin Ngayiwa na Mh. Mabula Magangila wamesema kongani hii ya viwanda ni hatua muhimu ya kukuza na kuchochea uchumi wa Wilaya ya Kahama na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment