KUPITIA COP30,TANZANIA KUVUNA DOLA MILIONI 447 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, December 17, 2025

KUPITIA COP30,TANZANIA KUVUNA DOLA MILIONI 447 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI



Na Hadija Omary Mazezele.


Tanzania inatarajia kunufaika na Dola za Marekani milioni 447.12 na Euro 500,000 kutokana na ushiriki wake katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika Belem, Brazil hivi karibuni.

Pia, Tanzania itapata kiasi cha Dola milioni 5 hadi 20 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupitia Mfuko wa Upotevu na Hasara.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe leo Desemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Kupokea Taarifa ya Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano COP 30, kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Prof. Msoffe ameeleza kuwa lengo la mkutano huo ni kuangaza na kujadili fursa mbalimbali katika kuisaidia jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na wadau.

Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kupitia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) ambapo imewezesha kujadiliwa na kukubalika kuwa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, kukubalika kwa hoja ya upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote (Mission 300).

“Tumeona hatua nzuri kupitia mkutano huo kama vile maamuzi ya nchi wanachama, kuwezesha Ofisi ya Kanda ya Santiago Network on Loss and Damage kufunguliwa Dar es Salaam nchini Tanzania. Aidha agenda ya nishati safi ya kupikia kimataifa ni ajenda inayopewa nguvu na uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

No comments:

Post a Comment