
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ametoa maelekezo kwa Bodi za Mabonde ya Maji Nchini kufanya tathmini ya kina ya vyanzo vyote vya maji ili kubaini hali yake halisi, ikiwemo uvamizi, uharibifu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhandisi Kundo ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake mkoani Songwe alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na serikali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Amesema tathmini hiyo itasaidia kujua ni vyanzo vipi vinaendelea kufanya kazi, vipi vimedhoofika na vipi vimekauka, hatua itakayoiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za kupanga mipango ya sasa na ya baadaye.
Amesisitiza kuwa vyanzo vya maji havikauki ghafla bali huonesha dalili na mwenendo, hivyo ni muhimu serikali kuwa na mfumo wa kisasa wa taarifa (database) unaosasishwa mara kwa mara ili kufuatilia mwenendo wa kila chanzo.
Aidha, Naibu Waziri ameagiza kubainishwa na kuibuliwa kwa vyanzo vipya vya maji ili kuwa na vyanzo mbadala, akisisitiza kuwa maandalizi ya miradi mipya yafanyike mapema kabla vyanzo vya awali havijakauka kabisa.
Kundo amesema hatua hizo zitawezesha Serikali kupanga vizuri usimamizi, ulinzi na uendelezaji wa vyanzo vya maji, kuongeza upatikanaji wa maji safi kwa wananchi na kuboresha elimu kwa umma kuhusu uhifadhi wa rasilimali za maji.


No comments:
Post a Comment