
Na Angela Maimbira, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameziagiza Halmashauri zote zenye makusanyo makubwa ya mapato ya ndani kuelekeza rasilimali hizo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na kutoa ajira kwa vijana.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Desemba 30, 2025, wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kilicholenga kujadili na kutathmini utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema uwekezaji katika miradi mikubwa ya kimkakati ni njia sahihi ya kuhakikisha mapato ya ndani yanatumika kwa tija, yakilenga kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan vijana kupitia ajira na fursa za kiuchumi.
Aidha, Prof. Shemdoe amesisitiza umuhimu wa Halmashauri kuwa na mipango madhubuti ya uwekezaji, kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha thamani ya fedha (value for money) inalindwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma.
Katika kikao hicho, Waziri Prof.Shemdoe amepokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali, akizitaka Idara, Vitengo na Taasisi kuendelea kuboresha usimamizi, uwajibikaji na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.




No comments:
Post a Comment