TANZANIA YANG’ARA KWENYE MKUTANO MKUU WA KUPAMBANA NA RUSHWA QATAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 16, 2025

TANZANIA YANG’ARA KWENYE MKUTANO MKUU WA KUPAMBANA NA RUSHWA QATAR


Kongamano kubwa zaidi duniani la kupambana na rushwa limemchagua Mhe. Naimi S.H. Aziz, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna kuwa Makamu wa Rais wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa (United Nations Convention against Corruption) kwa kipindi cha 2025-2027.

Uchaguzi huo umefanyika wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Nchi Wanachama uliofanyika tarehe 15 Desemba, 2025 jijini Doha, Qatar. Balozi Naimi Aziz amepewa jukumu la kumsaidia Rais wa Mkutano huo Hamad bin Nasser Al-Misnad, Rais wa Mamlaka ya Udhibiti, Uwazi na Uwajibikaji ya Qatar kuongoza Mkutano, kusimamia kazi za msingi za Mkutano Mkuu kama chombo kikuu cha kutunga sera kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba, kuongoza vikao, kuandaa ajenda, kuwezesha majadiliano ya utekelezaji wa Mkataba, na kufanya kazi na Ofisi ya Rais katika kusimamia na kukabiliana na rushwa duniani.

Katika Mkutano huo, ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila. Pia, umehudhuriwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CPA Charles Edward Kichere, na Maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma.

Wakati wa hafla ya ufunguzi wito ulitolewa kutumia teknolojia zinazoibuka katika vita dhidi ya ufisadi na kushughulikia uhusiano wake na uhalifu uliopangwa na uhalifu mwingine wa kifedha. 

Aidha, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock katika ujumbe wake alisema “Kuzuia na hatimaye kutokomeza rushwa ni jukumu la kila mmoja wetu. Tuna deni kwa watu tunaowahudumia.”

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres katika ujumbe wake kwa mtandao alisema “Rushwa siyo uhalifu usio na mwathirika. Inachochea migogoro, inatia mizizi ukosefu wa usawa, na inapoteza rasilimali zinazohitajika kulinda watu na sayari: Kila dola inayopotea kwa uhalifu wa kiuchumi ni dola iliyoibiwa kutoka kwa wale wanaopigania maisha bora ya baadaye.”

Ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kutoa ripoti utekelezaji wa Mkataba kwa kipindi cha 2023-2025.




No comments:

Post a Comment