TANZANIA YATOA RAI KWA RAIA WAKE WAISHIO MAREKANI "ZINGATIENI MASHARTI YA VIZA ZENU" - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, December 17, 2025

TANZANIA YATOA RAI KWA RAIA WAKE WAISHIO MAREKANI "ZINGATIENI MASHARTI YA VIZA ZENU"


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewataka Watanzania wote wanaosafiri kwenda Marekani kuzingatia kikamilifu masharti ya viza walizopewa, ikieleza kuwa kutofuata masharti hayo ndicho chanzo kikuu cha Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zilizowekewa vikwazo visivyokamilika vya kuingia nchini Marekani (partial restrictions and entry limitation)

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Desemba 17, 2025 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Serikali ya Marekani imetangaza kuiweka Tanzania katika kundi la nchi zenye vikwazo vya sehemu kuhusu kuingia nchini humo, hatua iliyotangazwa rasmi na Rais wa Marekani, Donald Trump, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Desemba 16, 2025. Hata hivyo Serikali ya Marekani imeeleza kuwa udhibiti huu si kamili na kwamba Watanzania watakaokidhi vigezo na masharti ya uhamiaji wataendelea kuruhusiwa kuingia nchini Marekani, kulingana na taratibu na tathmini zitakazotumika.

Tanzania imeeleza kuwa uamuzi huo umetokana na idadi kubwa ya Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani kushindwa kuzingatia masharti ya viza zao, hususan kwa kuishi nchini humo kwa muda mrefu zaidi ya ulioidhinishwa kisheria.

Taarifa ya Wakazi Waliopitiliza Muda (Overstay Report) imeonesha kuwa kiwango cha Watanzania wanaokaa nchini Marekani kinyume cha masharti ya viza kimekuwa kikubwa kuliko kiwango kinachokubalika chini ya sera za uhamiaji za Marekani.

“Taarifa hiyo ilionesha kuwa Tanzania imekuwa na kiwango kikubwa cha ukaaji wa zaidi ya muda kwa asilimia 8.3% kwa Visa zote za B-1/B-2 (Visa za biashara na utalii) na asilimia 13.97% kwa Visa za kundi la F, M na J (ambazo ni Visa za Wanafunzi, Mafunzo ya Ufundi, na programu za Kubadilishana yaani Exchange Programmes)”, imeeleza taarifa hiyo.

Viwango hivyo vimeelezwa kuwa juu zaidi ya kiwango cha kawaida kinachoruhusiwa, hali iliyosababisha Tanzania kujumuishwa katika orodha ya nchi zilizo chini ya vikwazo hivyo.

Pamoja na Tanzania, nchi nyingine zilizotajwa kuingia katika utaratibu huo ni Angola, Benin, Côte d’Ivoire, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe.

Aidha, Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa tayari imeanza na itaendelea kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Marekani kupitia Wizara za Mambo ya Nje za pande zote mbili, kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa haraka na wa kudumu ili Tanzania iondolewe katika kizuizi hicho.

Wakati jitihada hizo zikiendelea, Serikali imewasihi Watanzania wote wanaosafiri kwenda Marekani kuhakikisha wanazingatia masharti ya viza walizopewa, ikiwa ni pamoja na kuondoka nchini humo mara tu muda wa viza unapokamilika, ili kuepusha athari zaidi kwa hadhi ya nchi na kusaidia kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

No comments:

Post a Comment