TUNAIMARISHA GRIDI YA UMEME YA TAIFA ILI WANANCHI WOTE MPATE UMEME WA UHAKIKA – DKT. NCHEMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 19, 2025

TUNAIMARISHA GRIDI YA UMEME YA TAIFA ILI WANANCHI WOTE MPATE UMEME WA UHAKIKA – DKT. NCHEMBA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema baada ya Tanzania kuzalisha umeme wa kutosha kupitia miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), hatua inayofuata ni kuhakikisha wananchi wote wanapata umeme wa uhakika kupitia uimarishaji wa Gridi ya Taifa.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo tarehe 19 Desemba 2025 alipokuwa akizungumza na wananchi katika eneo la Somanga mkoani Lindi, baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa madaraja, ukarabati wa barabara, pamoja na maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa.

“Kulikuwa na masuala mawili makuu yaliyokuwa yakishughulikiwa na Serikali. Kwanza ilikuwa ni kufikisha miundombinu ya umeme ngazi ya mikoa, wilaya, kata na vijiji. Sasa kazi inayoendelea ni kusambaza umeme kwa wananchi kutoka katika vyanzo vya uzalishaji kama vile Julius Nyerere.

Ameeleza kuwa kwa sasa nchi ina ziada ya umeme, hivyo kazi iliyopo ni kuhakikisha umeme huo unawafikia wananchi kupitia uimarishaji wa Gridi ya Taifa.

Ameongeza kuwa, suala la kuwafikishia wananchi umeme limepewa pia kipaumbele katika Mpango wa Misheni 300, ambao Tanzania ilisaini mwezi Januari 2025. Kupitia mpango huo, Serikali inalenga kuwafikishia umeme wananchi wote ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Wizara ya Nishati inaendelea kuyatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuifungamanisha sekta ya nishati na maendeleo ya kiuchumi kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Mhe. Salome amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme katika mikoa hiyo ili wananchi wapate umeme wa uhakika na endelevu.

Mhe. Salome pia amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara mkoani Lindi, akieleza kuwa barabara hizo ni muhimu katika shughuli za uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia zinazopatikana katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Lindi pia inahusisha kutembelea mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Likong’o, inayojengwa kupitia Mradi wa kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), unaotarajiwa kutekelezwa katika kijiji hicho.

Kutoka Wizara ya Nishati, ziara hiyo pia imehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio.

No comments:

Post a Comment